Rodrygo aeleza simu moja tu ilivyoua dili lake Barcelona
Muktasari:
- Akizungumza na gazeti la Diario AS, Rodrygo amekiri kuwa Barcelona ilikaribia kumsajili kabla ya Real Madrid, lakini alifanya uamuzi wa kukataa mpango huo na kuamua kujiunga na magwiji wa mji wa Madrid.
Kwa mara ya kwanza, winga wa Real Madrid, Rodrygo Silva de Goes amefichua siri yake ya kukaribia kusajiliwa na FC Barcelona, akitokea nyumbani kwao Barazil alipokuwa akiitumikia klabu ya Santos.
Akizungumza na gazeti la Diario AS, Rodrygo amekiri kuwa Barcelona ilikaribia kumsajili kabla ya Real Madrid, lakini alifanya uamuzi wa kukataa mpango huo na kuamua kujiunga na magwiji wa mji wa Madrid.
Katika mahojiano hayo, Rodrygo amefichua kuwa uhamisho wake kwenda Barca ulikuwa tayari umekamilika, lakini alibadilisha uamuzi mara baada ya kupokea simu kutoka kwa mabosi wa Real Madrid.
"Kabla ya kusaini Real Madrid, kila kitu kilikuwa tayari na nilikuwa nimeshasaini Barcelona. Ni kweli. Lakini baba yangu aliniambia kuwa Madrid walitupigia simu na nikapaswa kuchagua. Kwangu mimi ilikuwa rahisi sana. Nilijua nilichotaka na ndoto yangu ilikuwa nini. Sikusita hata kidogo. Na sasa niko hapa," amesema.
"Nilikuwa Santos na nilikuwa naanza kucheza vizuri. Barca walinifuata, na nimekuwa nikisema kuwa ni klabu kubwa na nina heshima kubwa kwao. Lakini Real Madrid ilikuwa ndoto yangu, na uamuzi wangu ulikuwa rahisi. Sikuweza kungoja zaidi, na muda ulipofika, tulifanya kila kitu kwa njia sahihi." ameongeza.
Rodrygo alijiunga na Real Madrid mwaka 2019 akitokea Santos kwa ada ya uhamisho inayoripotiwa kuwa Pauni 45 milioni. Tangu wakati huo, ameichezea Madrid mechi 278, akifunga mabao 68 na kutoa pasi za mabao 53.
El Clásico ya Oktoba 26, 2025 inatarajiwa kuwa kipimo kikubwa kwa vikosi vyote, huku Rodrygo na wenzake wakitaka kulipiza kisasi kwa vipigo vya msimu uliopita.
BARCELONA WAJE TU, TUPO TAYARI KWA EL CLÁSICO
Winga wa Real Madrid, Rodrygo, ameonyesha kuwa tayari kuelekea mchezo wa El Clásico dhidi ya wapinzani wao, FC Barcelona, utakaopigwa Oktoba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabéu. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana msimu huu wa Ligi ya LaLiga.
Msimu uliopita, Barcelona chini ya kocha Hansi Flick iliibuka na ushindi katika mechi zote mbili dhidi ya Real Madrid. Timu hizo zilikutana mara nne katika mashindano tofauti, na kila mara Barcelona iliibuka kidedea.
Akizungumza na gazeti la Diario AS, Rodrygo amekiri kuwa, Real Madrid ilipata wakati mgumu dhidi ya Barca msimu uliopita, lakini amesisitiza kuwa kikosi chao kiko tayari kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanashinda mbele ya mashabiki wao katika uwanja wa Santiago Bernabéu.
"Ni bora tusahau ya msimu uliopita. Tunajua hatukuwa kwenye kiwango bora, hasa katika El Clásico," amesema Rodrygo.
"Hatukuwa na raha dhidi yao. Ni kweli kwamba msimu uliopita wao walitushinda mara zote nne, lakini pia lazima tukubali kuwa sasa wana kikosi bora zaidi na kujiamini zaidi. Lakini nasi pia tuna timu nzuri. Itakuwa mechi ngumu, lakini tunacheza nyumbani mbele ya mashabiki wetu, na lazima tuonyeshe uwezo wetu, tukipanga kila kitu vizuri ili kuwashinda bila kujali hali yoyote. Tunatakiwa kutambua tuko nyumbani."
Cha kufurahisha, mechi ya kwanza kwa vigogo hao msimu uliopita ilichezwa Oktoba 26, 2024 kwenye uwanja Santiago Bernabeu, ambapo Barcelona iliitandika Real Madrid mabao 4-0.
Kwa sasa, Real Madrid inaongoza msimamo wa La Liga ikiwa na pointi 21 baada ya mechi 8, huku Barcelona ikifuatia kwa karibu ikiwa na pointi 19 katika nafasi ya pili.