Bao la jioni laisukuma DR Congo nje Afcon
Muktasari:
- Matokeo hayo, ambayo yanaiacha DR Congo ikiendelea kusaka ushindi wake wa kwanza kabisa dhidi ya Algeria, yalikuwa machungu kwa timu hiyo ya Afrika ya Kati na hivyo kutupwa nje ya mashindano katika hatua ya 16 bora.
MARRAKESH, MOROCCO: BAO la Adil Boulbina alilofunga dakika za mwisho za muda wa nyongeza lilitosha kuamua mechi ngumu dhidi ya DR Congo na kuifanya Algeria kufuzu kwenda robo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 baada ya ushindi wa bao 1-0 uwanjani Stade Moulay El Hassan.
Akipigwa pasi upande wa kushoto na mchezaji mwenzake aliyeingia kutokea benchini Ramiz Zerrouki, Boulbina alimpita kwa kasi beki aliyekuwa amechoka Aaron Wan-Bissaka, akakata kuelekea ndani na kupiga shuti kali la mguu wa kulia ambalo halikuweza kuzuilika. Mpira ulipaa juu ya kipa Lionel Mpasi na kugonga chini ya mwamba wa lango kabla ya kuingia, likiwa ndilo bao pekee la mchezo.
Matokeo hayo, ambayo yanaiacha DR Congo ikiendelea kusaka ushindi wake wa kwanza kabisa dhidi ya Algeria, yalikuwa machungu kwa timu hiyo ya Afrika ya Kati na hivyo kutupwa nje ya mashindano katika hatua ya 16 bora.
Baada ya kupambana kwa nguvu katika mchezo uliokuwa wa vuta nikuvute mjini Rabat, timu zote zilionekana kama wangefika kwenye mikwaju ya penalti, kabla ya Boulbina kuibuka na bao la kushtukiza.
Katika mchezo uliokuwa na nafasi chache, huku safu za ulinzi zikitawala, gwiji wa soka wa Ufaransa, Zinedine Zidane alikuwa tena uwanjani kumshuhudia mwanawe, Luca akihifadhi rekodi ya kutoruhusu bao kwa mara ya nne katika mashindano haya kwa Les Fennecs.
Kwa kuwa na safu ya ulinzi imara kiasi hicho, mabingwa wa Afcon 2019 watajipa matumaini makubwa ya kuwadhibiti wapinzani wao wa robo fainali, Nigeria, wanaofunga mabao mengi, watakapokutana mjini Marrakesh siku ya Jumamosi.