Kaa chonjo… Ni robo fainali ya vigogo Afrika
Muktasari:
- Kadri mashindano haya makubwa yanavyozidi kushika kasi, kuingia kwenye mtoano kumeendelea kudhihirisha tofauti ndogo sana zilizopo kati ya timu zinazoendelea na zile ambazo zimefungashiwa virago. Hii ni hatua nzuri katika ukuaji wa soka la Afrika.
MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea nchini Morocco sasa imeingia katika hatua ya robo fainali, huku mechi za hatua ya 16 bora zikitamatika jana, Jumanne kwa ushindani wa aina yake kutoka kwa vigogo wa soka la Afrika.
Kadri mashindano haya makubwa yanavyozidi kushika kasi, kuingia kwenye mtoano kumeendelea kudhihirisha tofauti ndogo sana zilizopo kati ya timu zinazoendelea na zile ambazo zimefungashiwa virago. Hii ni hatua nzuri katika ukuaji wa soka la Afrika.
Kabla ya mechi za jana (Jumanne) usiku, kulikuwa na timu sita zilizojikatia tiketi ya kucheza robo fainali, kila moja ikipitia njia tofauti lakini zote zikiwa na lengo moja tu ambalo ni kusaka ufalme wa Afrika katika michuano hii ya 35.
WALITANGULIA MAPEMA
Senegal ilikuwa taifa la kwanza kufuzu hatua ya robo fainali. Mabingwa hao wa zamani wa Afrika waliendeleza rekodi yao ya kutopoteza katika michuano hii baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Sudan.
Mali ikiwa na kipa wa Yanga, Djigui Diarra iliwafuata kwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kupambana kufuatia kuing’oa Tunisia kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya kutoka sare ya bao1-1 katika dakika 90, licha ya kucheza sehemu kubwa ya mchezo huo wakiwa pungufu kwa mchezaji mmoja.
Wenyeji wa michuano hiyo, Morocco, waliwafurahisha mashabiki wao wa nyumbani jijini Rabat baada ya kuifunga Tanzania kwa bao 1–0. Katika mchezo ambao uligubikwa na utata kufuatia tukio la Taifa Stars kunyimwa mkwaju wa penalti baada ya Iddy Seleman ‘Nado’ kuangushwa katika eneo la hatari huku Brahim Díaz akifunga bao la ushindi.
Matokeo hayo hayakuendelea tu kuiweka Morocco kwenye mbio za ubingwa, bali pia yaliamsha matumaini makubwa kwamba huenda hiki kikawa kizazi kitakachovunja ukame wa miaka 50 bila taji la AFCON.
Baadaye Jumapili, Cameroon iliongeza idadi ya waliofuzu robo fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya Afrika Kusini. Mabingwa hao mara tano wa Afrika walionyesha kwa mara nyingine uzoefu wao mkubwa wa michezo ya mtoano, wakipata ushindi katika mchezo uliokuwa mkali na wa kusisimua.
Sasa Cameroon inatarajiwa kukutana na wenyeji Morocco katika robo fainali inayotajwa kuwa miongoni mwa mechi kali zaidi za hatua hiyo.
JUMATATU ILIKUWA MOTO
Hatua ya 16 bora iliendelea Jumatatu usiku kwa mechi nyingine zilizotoa picha iliyo wazi zaidi ya timu zitakazounda robo fainali.
Misri iliing’oa Benin kwa ushindi wa mabao 3–1 baada ya dakika 120 za mchezo. Mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa kabla ya nyota wao Mohammed Salah kufunga bao la mwisho katika sekunde za mwisho za muda wa nyongeza, akionyesha umuhimu wake katika nyakati za maamuzi na kuendeleza matumaini ya Misri kutwaa taji lao la nane.
Nigeria nao walithibitisha ubora wao kwa kuichapa Msumbiji mabao 4–0, katika mchezo uliotawaliwa na Super Eagles. Victor Osimhen alikuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kufunga mabao mawili na kuonyesha kwa nini anatambuliwa kama mmoja wa washambuliaji hatari barani Afrika.
ROBO FAINALI
Robo fainali za mwaka huu zimepangwa kuchezwa kwa siku mbili mfululizo, Ijumaa ya Januari 9 na Jumamosi Januari 10, 2026, katika viwanja vinne tofauti nchini Morocco, hali inayoongeza mvuto na upana wa mashindano haya makubwa ya Afrika.
Mechi ya kwanza ya robo fainali itawakutanisha Mali dhidi ya Senegal katika Uwanja wa Tangier Grand jijini Tangier. Mechi hii ni ya majirani wa Afrika Magharibi huku Senegal ikibebwa na uzoefu huku Mali ikija na morali baada ya ushindi wa kishujaa dhidi ya Tunisia.
Katika robo fainali ya pili, macho yote yataelekezwa Rabat ambako Cameroon watakutana na wenyeji Morocco katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah. Hii ni mechi inayobeba uzito wa kihistoria, ikiwakutanisha mabingwa mara tano wa Afrika dhidi ya taifa linalotafuta taji lake la kwanza la AFCON baada ya miaka 50.
Faida ya kucheza nyumbani inatarajiwa kuwa silaha muhimu kwa Morocco huku wakitegemea sapoti kubwa ya mashabiki wao pamoja na ubora wa kikosi chao. Cameroon, kwa upande mwingine, wanaingia wakiwa na uzoefu mkubwa wa mechi za mtoano na uwezo wa kustahimili presha katika nyakati muhimu.
Jumamosi, Nigeria itashuka dimbani katika Uwanja wa Marrakesh kuikabili dhidi ya Algeria au DR Congo ambao walicheza jana usiku. Super Eagles wanaingia katika robo fainali hii wakiwa na kujiamini baada ya ushindi mkubwa wa mabao 4–0 dhidi ya Msumbiji, huku Victor Osimhen akionekana kuwa katika kiwango bora.
Hata hivyo, Nigeria wanajua kuwa katika hatua ya robo fainali hakuna mpinzani mdogo na timu yoyote itakayokutana nao itakuwa na hamu kubwa ya kuandika historia. Hii inafanya mechi hiyo kuwa ya tahadhari na umakini mkubwa kwa pande zote mbili.
Robo fainali ya mwisho itachezwa Jumamosi usiku katika Uwanja wa Adrar jijini Agadir, ambapo Misri watakutana na mshindi kati ya Ivory Coast dhidi ya Burkina Faso. The Pharaohs walilazimika kwenda dakika 120 kabla ya kuiondoa Benin, ushindi uliowaongezea morali na kuonyesha tabia yao ya kupambana hadi dakika ya mwisho.
Kwa ujumla, robo fainali za AFCON 2025 zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali, presha kubwa na soka la kiwango cha juu, huku timu nne pekee zikitarajiwa kufuzu nusu fainali. Mashabiki wa soka barani Afrika sasa wanasubiri kwa hamu kuona ni nani atakayefanikiwa kusonga mbele na kuendelea kuishi ndoto ya kutwaa taji la AFCON 2025.