Babu Ferguson akubali mziki wa Lammens
Muktasari:
- Mbelgiji huyo wakati anasajiliwa na Man United dirisha lililopita la majira ya kiangazi alionekana kama anakwenda tu kuongeza idadi ya watu kwenye timu hiyo ya Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: SIR Alex Ferguson amesifu kiwango cha kipa Senne Lammens akisema anapiga kazi si mchezo na hivyo kujitengenezea nafasi ya kuanza golini kwenye kikosi cha Manchester United.
Mbelgiji huyo wakati anasajiliwa na Man United dirisha lililopita la majira ya kiangazi alionekana kama anakwenda tu kuongeza idadi ya watu kwenye timu hiyo ya Old Trafford.
Nafasi ya kipa imekuwa tatizo kubwa kwenye kikosi cha Man United kwa miaka kadhaa, huku Andre Onana akishindwa kumaliza tatizo hilo na mwenyewe alikuwa tatizo kwa miaka yake miwili katika kikosi hicho kabla ya kutolewa kwa mkopo dirisha lililopita.
Kocha Ruben Amorim baada ya kuchoshwa na Onana, aliamua kumpa nafasi Altay Bayindir, ambaye pia alimwangusha na hivyo kuamua kutumia Pauni 18 milioni kunasa saini ya Lammens kutoka Royal Antwerp.
Kipa huyo Mbelgiji alianza kuichezea Man United kwenye mechi dhidi ya Sunderland na alizuia nyavu zake zisiguswe na kisha alisimama imara kabisa golini kusaidia ushindi dhidi ya Liverpool huku Man United ikicheza mechi tano bila ya kupoteza na kupanda nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Ferguson amesema: "Safi, kuna dalili nzuri, kocha ameonyesha kuna dalili nzuri. Yule kipa amekuwa na kiwango kizuri, ni mechi tatu tu au nne, lakini ameonyesha ni kipa mzuri.
"Bila shaka, Mbeumo na Cunha, wachezaji wapya kutoka Wolves na Brentford, wameongeza kitu. Natumaini kocha atapata mafanikio kwa sababu Man United inahitaji mafanikio tu. Dalili ni nzuri. Nadhani kushinda mechi mfululizo ni kitu ambacho Man United kinapaswa kuwapo kila wakati. Lakini, bado kuna nafasi ya kuwa bora zaidi, tunapaswa kusubiri na kuwa na imani, kwa sasa hata wachezaji wameanza kucheza kwa kufurahia."
Lammens alicheza mechi 52 tu kwenye Belgian Pro League kabla ya kuhamia kwenye Ligi Kuu England, lakini kocha Amorim ameonyesha imani kubwa kwa kipa huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye ameonyesha kiwango bora kwenye safu ya ulinzi ya miamba hiyo.
Hata Ferguson katika kipindi chake alitegemea makipa kumpa mataji mengi na makipa waliombeba kocha huyo mkongwe alikuwa Peter Schmeichel na Edwin van der Sar.
Kipa mwingine aliyempa mafanikio makubwa Ferguson ni David de Gea. Kipa huyo Mhispaniola alikuwa namba moja wa Man United kwa zaidi ya muongo mmoja, akishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka mara nne, kabla ya kuondoka mwaka 2023.