Tuchel kichwa kinauma!
Muktasari:
- Mjadala uliopo ni kwamba atawezaje kuwajumuisha Eberechi Eze, Cole Palmer, Morgan Rogers, Anthony Gordon na Marcus Rashford kwenye kikosi kimoja endapo kama kila mmoja atakuwa kwenye kiwango bora hadi kufikia wakati huo? Bila shaka wachezaji hao kila mmoja atajaribu kucheza kwenye kiwango chake bora walau kuwamo kwenye ndege itakayoelekea kwenye fainali hizo na kikosi cha Three Lions. Kazi ipo.
LONDON, ENGLAND: MIEZI minne kutoka sasa, England itarusha kete yake ya kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa kumenyana na Croatia mjini Dallas, Marekani. Lakini, shughuli anayo kocha wa England, Mjerumani Thomas Tuchel juu ya uteuzi wa kikosi chake, nani abaki nyumbani nani aende kwenye fainali hizo. Kichwa kinampasuka.
Mjadala uliopo ni kwamba atawezaje kuwajumuisha Eberechi Eze, Cole Palmer, Morgan Rogers, Anthony Gordon na Marcus Rashford kwenye kikosi kimoja endapo kama kila mmoja atakuwa kwenye kiwango bora hadi kufikia wakati huo? Bila shaka wachezaji hao kila mmoja atajaribu kucheza kwenye kiwango chake bora walau kuwamo kwenye ndege itakayoelekea kwenye fainali hizo na kikosi cha Three Lions. Kazi ipo.
Safu ya ulinzi; Jordan Pickford bado ni kipa namba moja wa England na hana mpinzani wa karibu, licha ya makosa kadhaa ya kutia wasiwasi katika wiki za hivi karibuni. Lakini, Tuchel shughuli inayomkabili ni kwenye kutambua mabeki wa kumlinda Pickford. Nani anafaa? Ndani ya miezi 18 iliyopita, England imetumia wachezaji 10 tofauti kwenye safu hiyo.
Tuchel anampenda Nico O’Reilly na alicheza vizuri kama beki wa kushoto kipindi cha vuli. Lakini, kimsingi yeye ni kiungo chipukizi na amerudi kucheza nafasi hiyo Manchester City. Kwenye beki ya kushoto kuna vita pia itakayomhusisha pia Lewis Hall na huenda Myles Lewis-Skelly, Tino Livramento na Djed Spence nao wakashindania nafasi kama ilivyo kwa Luke Shaw na Dan Burn. Kwenye beki ya kati, John Stones anaweza kucheza sambamba na beki mwenye utulivu Marc Guehi, ambaye wanacheza pamoja Man City.
Lakini kuna Ezri Konsa na Reece James wanaweza kujumuishwa pia sambamba na Harry Maguire, anayecheza kwa kiwango bora kabisa kwenye kikosi cha Manchester United kwa sasa. Kuhusu Trent Alexander-Arnold naye atamsikilizia tu kocha Tuchel.
Safu ya kiungo; England ina bahati kuwa na Declan Rice, ambaye ni thabiti kwa klabu yake na taifa. Lakini nafasi ya kiungo mkabaji (No.6) inaleta wasiwasi. Elliot Anderson wa Nottingham Forest alikuwa bora kabla ya Krismasi, lakini kiwango chake kimeshuka huku timu ikipambana dhidi ya kushuka daraja. Jordan Henderson wa Brentford hataanza mechi za Kombe la Dunia, hata kama atachaguliwa kwa uzoefu wake. Lakini, kuna orodha ya viungo wengine kama Adam Wharton wa Crystal Palace, Curtis Jones wa Liverpool, Morgan Gibbs-White wa Forest na Conor Gallagher wa Tottenham Hotspur. Tuchel pia anamkubali James Garner wa Everton, huku Kobbie Mainoo akirudi kwenye hesabu baada ya kurejea uwanjani kwa Man United na kufanya vizuri tangu apewe nafasi na kocha Michael Carrick.
Safu ya ushambuliaji; Bado kila kitu kinamzunguka Harry Kane. Zaidi yake, mambo ni ya kubahatisha. Je, katika Kombe la Dunia ungependa England ianze na Ollie Watkins, Ivan Toney, Liam Delap, Dominic Solanke, Danny Welbeck au Dominic Calvert-Lewin kama mshambuliaji mkuu? Sio kitu rahisi kama Kane atakuwa hana shida yoyote ya kiafya. Kwenye winga na Namba 10, England imejaa vipaji vingi.
Bukayo Saka ni chaguo la uhakika kwa England. Mbali yake yupo Noni Madueke, Jarrod Bowen, Morgan Rogers na Anthony Gordon. Kwenye Namba 10 mambo ni moto zaidi, hapo kuna mastaa kama Eze, Phil Foden, Rashford, Palmer, Jude Bellingham na Jack Grealish endapo kama atapona majeraha yake kwa wakati na Tuchel akaamua kumfikiria kuwamo kwenye kikosi chake. Katika wiki zijazo, Tuchel ataendelea kutembelea viwanja mbalimbali kuona ni wachezaji gani ambao atahitaji kuwajumuisha kwenye kikosi chake kwa ajili ya fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico katika majira yajayo ya kiangazi.