Arteta: Gyokeres? Bado kidogo tulieni
Muktasari:
- Ingawa Arsenal ilipata pointi tatu dhidi ya Man United katika Uwanja wa Old Trafford Jumapili, Gyokeres, aliyejiunga nao dirisha hili, hakuonyesha kiwango bora.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amesema ushindi wa Arsenal wa 1-0 dhidi ya Manchester United ulikuwa kama 'mchezo wa mpira wa kikapu' na hali hiyo haikumpa nafasi Viktor Gyokeres kuonyesha makali yake.
Ingawa Arsenal ilipata pointi tatu dhidi ya Man United katika Uwanja wa Old Trafford Jumapili, Gyokeres, aliyejiunga nao dirisha hili, hakuonyesha kiwango bora.
Katika dakika 60 ambazo mchezaji huyo wa zamani wa Brighton alicheza, hakutengeneza nafasi yoyote, hakupiga mpira wowote, aligusa mpira mara tatu tu katika kisanduku cha Man United na alipata mpira mara tatu tu alipokuwa akigombania.
Hata hivyo, kocha wa Arteta amemtetea akisema: "Nafikiri kulikuwa na nyakati saba au nane mpira ulikuwa wazi kwetu kuweza kushambulia na kupiga golini lakini tulishindwa kufanya hivyo, tukaacha ukapotea kisha mchezo ukawa kama wa mpira wa kikapu.”
"Alifanya mambo mengi vizuri sana. Alionekana hasa katika shinikizo na namna tulivyokuwa tunashambulia, hatukumpa huduma ya kutosha kwa kupeleka mipira katika maeneo sahihi ili kuweza kutumia ubora wake, lakini kwa jumla, kuja Old Trafford na kuondoka ukiwa umeibuka na ushindi wako wa kwanza kama mchezaji mpya wa Arsenal, ni mwanzo mzuri."
Mashabiki wa Arsenal walikuwa wakilia kwa muda mrefu, klabu hiyo kumtafutia mshambuliaji bora na baada ya hilo kufanyika kwa kusajiliwa Gyokeres kwa Pauni 64 milioni dirisha hili, wengi wanaamini tatizo sasa limekwisha na wanaweza kushinda taji lao la kwanza la Ligi Kuu England tangu mwaka 2004.
Hata hivyo, katika mechi yake ya kwanza, staa huyu, 27, hajaonyesha kiwango bora kama ilivyotarajiwa na wengi na ana nafasi ya kurekebisha makosa yake katika mchezo wa pili wa EPL msimu huu na Arsenal itakutana na Leeds United, iliopanda daraja msimu huu.