Arteta aukatia tamaa ubingwa EPL, ashuka na mastaa Arsenal
Muktasari:
- Na jambo hilo limewafanya wacheza kamari sasa kuamini moja kwa moja Liverpool inakwenda kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya Arsenal kuchapwa na West Ham United uwanjani kwao Emirates.
LONDON, ENGLAND: KOCHA, Mikel Arteta kwa hasira amewashambulia kwa maneno mastaa wake wa Arsenal akiwashutumu kwamba hawana viwango vya kuwa mabingwa.
Na jambo hilo limewafanya wacheza kamari sasa kuamini moja kwa moja Liverpool inakwenda kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya Arsenal kuchapwa na West Ham United uwanjani kwao Emirates.
Na bosi wa Arsenal, Arteta kwa hasira alisema: “Nimekasirika sana. Natumaini pia timu imechukia. Kwa uchezaji ule yani hatukuwa kabisa kwenye viwango vya kushinda taji la Ligi Kuu.”
Mtokea benchini Myles Lewis-Skelly alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Mohammed Kudus — hivyo kuifanya Arsenal kuwa na kadi tano nyekundu msimu huu.
Alipoulizwa kama mbio za ubingwa kwa Arsenal zimefika ukomo, Arteta alisema: “Haupo tena kwenye mikono yetu. Nimechukizwa sana kwasababu mambo yalikuwa kwenye mikono yetu, lakini sasa hayapo tena. Yatupaswa kujiangalia kwenye kioo kutambua kile tunachoweza kukifanya kwa ubora. Tujione tuna dhamira gani na kile tunachotaka kukifanya.”
Vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool ilikuwa na mechi ngumu dhidi ya Manchester City, Jumapili na ushindi kwa vijana wa Arne Slot utawafanya kuongoza ligi hiyo kwa pointi 11.
Kwenye mchezo wao, Arsenal imepiga mashuti mawili tu kulenga goli, huku kocha Arteta alimpanga kiungo Mikel Merino kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati baada ya Kai Havertz, Bukayo Saka, Gabriel Martinelli na Gabriel Jesus kuwa majeruhi.
Arteta aliongeza: “Hata kama tungepiga mashuti 20, sijaona kabisa kama tulikuwa kwenye viwango vilivyohitajika. Tulishindwa kabisa kuwa kwenye kasi ya mchezo.
“Sitaki kusema kukosekana kwa mastraika, ninachojaribu kusema ni wachezaji kukosa viwango. Hiki kiwango chetu hakitoshi. Lazima upambane na unahitaji kuwa na viwango vya juu.”
Kipigo hicho cha bao 1-0 lililofungwa na Jarrod Bowen lilitosha kuhitimisha mechi 15 kucheza bila ya kupoteza.
Nahodha wa Washika Bunduki hao wa London, Martin Odegaard alikubaliana na kocha Arteta akisema: “Kiwango hakikuwa kizuri. Ni pigo kubwa, inahuzunisha sana. Nimekosa wachezaji wetu ambao ni wazuri. Hatukuwa vizuri hata kwenye fowadi.”