Arteta atamba usajili dirisha kubwa

Muktasari:
- Ikiwa ni mwaka wa tano sasa tangu alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo Desemba 2019, Arteta ameshuhudia panda shuka kwenye kikosi hicho cha Arsenal , ikiwamo msimu mmoja wa kumaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi na ule wa kushinda ubingwa wa taji la Kombe la FA.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amesisitiza dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi litakwenda kuwa kitu kikubwa sana kwenye kikosi chake hicho cha Emirates.
Ikiwa ni mwaka wa tano sasa tangu alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo Desemba 2019, Arteta ameshuhudia panda shuka kwenye kikosi hicho cha Arsenal , ikiwamo msimu mmoja wa kumaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi na ule wa kushinda ubingwa wa taji la Kombe la FA.
Septemba 2020, cheo chake kilibadilika kutoka kuwa kocha mkuu hadi kuwa meneja wa miamba hiyo ya Emirates na hapo, Arsenal alitengeneza mpango wa miaka mitano wa kuibadili timu hiyo kuitoa kuwa ya kawaida na kuifanya ya kushindania mataji makubwa, ikiwamo Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Madirisha manne ya uhamisho wa majira ya kiangazi yamepita, ambapo Arsenal imejaribu kujijenga ambapo kocha Arteta ameamua kuweka mipango yake kwenye timu.
Na dirisha lake la tano la majira ya kiangazi limebakiza miezi miwili tu na Arsenal inataka kutumia usajili huo kama fursa ya kutengeneza kikosi ambacho kitakuwa na nguvu ya kubeba ubingwa baada ya msimu huu kuelekea kumaliza kwenye nafasi ya pili kwa msimu wa tatu mfululizo.
Dirisha lijalo la majira ya kiangazi, Arsenal kitu itafanya ni kusajili wachezaji ambao inaamini ndio wanaookosekana kwenye kuifanya timu hiyo kuwa na nguvu kubwa kwenye kubeba mataji.
Usajili wa kwanza umeshafanyika, mkurugenzi mpya wa michezo, Andrea Berta, ambaye ataanza kazi huko London Colney wiki hii katika kuweka michakato vizuri na kuhakikisha anampatia Arteta Namba 9 wa mataji.
Swali lililopo je, Berta atalipa Pauni 100 milioni au zaidi kumnasa staa wa Newcastle United, Alexander Isak, 25? Au atakuwa tayari kulipa mkwanja zaidi wa kunasa saini ya Hugo Ekitike,22 wa Eintracht Frankfurt?
Atakubali kulipa kati ya Pauni 50 milioni au Pauni 60 milioni kwa ajili ya kunasa saini ya straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres, 26, au Mbrazili wa Wolves, Matheus Cunha, 25?
Arsenal inahitaji straika wa kuja kuwapa mataji. Berta akikosa huduma za mastraika hao wa juu, atafungua pochi kulipa kati ya Pauni 70 milioni hadi Pauni 80 milioni kumchukua straika wa Red Bull Leipzig, Benjamin Sesko, 21?
Vyovyote itakavyokuwa, Arteta alisema dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi litakuwa bab kubwa.
Alisema: “Itakwenda kuwa bab’kubwa na tunalisubiri kwa hamu. Kwa namna ambavyo tulipanga madirisha matano ya kwanza ya majira ya kiangazi, hili litakwenda kuwa bab kubwa kwa sababu litakuwa na malengo tofauti.
“Mwanzoni kulikuwa na wachezaji wengi wenye mikataba ya miaka mitatu, minne au mitano. Hii inakwenda kuwa kubwa kwa sababu tumeshatengeneza msingi mzuri na kwamba tunachofanya sasa ni kuboresha timu.”
Berta, 53, atafanya kazi na mkurugenzi mkuu Richard Garlick, makamu mwenyekiti Tim Lewis, mmiliki mwenza Stan na Josh Kroenke na mkurugenzi wa soka uratibu, James King.