Arteta aogopa mziki wa Slot
Muktasari:
- Liverpool imevunja rekodi ya uhamisho wa Uingereza kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu mara mbili tofauti, kwanza ilipomsajili kiungo Florian Wirtz kwa Pauni 116 milioni, kabla ya kutoa Pauni 130 milioni kunasa saini ya straika Alexander Isak.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amesema Liverpool imesajili kikosi bora kabisa ikitumia zaidi ya Pauni 400 milioni kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwaka huu na kusema mbio za ubingwa zitakuwa ngumu.
Liverpool imevunja rekodi ya uhamisho wa Uingereza kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu mara mbili tofauti, kwanza ilipomsajili kiungo Florian Wirtz kwa Pauni 116 milioni, kabla ya kutoa Pauni 130 milioni kunasa saini ya straika Alexander Isak.
Miamba hiyo ya Anfield inayonolewa na Arne Slot imefanya usajili pia kwa kuwanasa Jeremie Frimpong, Milos Kerkez, Giovanni Leoni na Hugo Ekitike na kutengeneza kikosi cha kibabe kabisa katika mbio za ubingwa wa ligi.
Arsenal yenyewe pia imefanya usajili mkubwa kwenye dirisha hili, ikitumia zaidi ya Pauni 250 milioni kunasa mastaa wapya. “Wao ni timu yenye nguvu hakika,”€ alisema Arteta akiwazungumzia Liverpool wakati alipozungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Nottingham Forest iliyopaswa kufanyika jana.
“Wamefanya usajili wa wachezaji wawili ghali sana (Isak na Wirtz). Wana timu yenye nguvu sana, hivyo tunapaswa kujitazama sana uwezo wetu kama tunataka kuwa bora kuliko wao.”€
Arsenal ilimaliza msimu wa 2024-25 pointi 10 nyuma ya Liverpool, iliyobeba ubingwa wakati kocha Slot ukiwa ni msimu wake wa kwanza.
Na kwenye usajili wa Isak, Liverpool imefanikiwa kumsajili straika aliyeshika namba mbili kwa kufunga kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, nyuma ya Mohamed Salah, ambaye ni mkali wa Anfield, huku Wirtz huko alikotokea kwenye Bundesliga, alichangia mabao 23 katika mechi 31 alizocheza kwenye mikikimikiki ya Bundesliga.