Arsenal yatoa onyo Ulaya

Muktasari:
- Huo ulikuwa usiku matata kabisa kwa Arsenal katika historia yao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikipata ushindi mkubwa, kuzidi ule iliyowahi kupata Arsenal isiyofungika ya Arsene Wenger, ilipoikamua Inter Milan 5-1 uwanjani San Siro, Novemba 2003 – Thierry Henry alipowavuruga kina Javier Zanetti na wenzake.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL ni kama imeshatinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kushusha kipigo kizito cha mabao 7-1 kwa PSV Eindhoven katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huko Uholanzi usiku wa Jumanne.
Huo ulikuwa usiku matata kabisa kwa Arsenal katika historia yao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikipata ushindi mkubwa, kuzidi ule iliyowahi kupata Arsenal isiyofungika ya Arsene Wenger, ilipoikamua Inter Milan 5-1 uwanjani San Siro, Novemba 2003 – Thierry Henry alipowavuruga kina Javier Zanetti na wenzake.
Miaka 22 baadaye, Arsenal imekwenda ugenini huko PSV na kwenda kufanya balaa la ushindi wa mabao saba.
Kwa kifupi tu, Arsenal imekuwa timu ya kwanza kufunga mabao saba kwenye mechi ya mtoano katika mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mechi za ugenini.
Wakati Wenger alikuwa na Henry, Robert Pires na Freddie Ljungberg kwenye kikosi chake, Arteta alifanya maajabu yake kwa kushinda idadi kubwa hiyo ya mabao bila ya kuwa na straika wa asili na kumtumia kiungo wa kati, Mikel Merino kama mshambuliaji wake wa kati.
Kiungo huyo Mhispaniola alitikisa nyavu kwenye mechi hiyo sambamba na Jurrien Timber, Ethan Nwaneri, Leandro Trossard, Riccardo Calafiori na Martin Odegaard, aliyefunga mara mbili kuimaliza PSV.
Hiyo ilikuwa ya mara ya kwanza pia kwa Arsenal kufunga mabao yanayozidi matatu kwenye mechi ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyocheza ugenini. Bila ya kujali kwamba Arsenal ilikuwa ikiomba Bukayo Saka na Gabriel Martinelli wacheze kwenye mechi hiyo, bila ya shaka watahitaji huduma yao kutokana na mechi ya robo fainali, ambapo wanaweza kuwa na mtihani kuikabili Real Madrid au Atletico Madrid mwezi ujao.
Kabla ya usiku wa Jumanne, mechi ya mwisho ya Arsenal na PSV ilikuwa Desemba 2023 ilimalizika kwa sare ya 1-1. Lakini, miezi 15 baadaye, PSV ikiwa uwanjani Philips Stadion, iliikaribisha Arsenal kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora na kilichowakuta, hawakitasahau kwenye historia yao. Arsenal sasa inasubiri tu mechi ya marudiano Jumatano ijayo kukamilisha ratiba, huku ikisubiri kuona itakabiliana na timu gani kwenye robo fainali.
TAKWIMU ZA MCHEZO HUO PSV vs ARSENAL
-Mashuti golini: PSV 2, Arsenal 8
-Mashuti yote: PSV 12, Arsenal 15
-Mashuti kuzuiwa: PSV 4, Arsenal 3
-Umiliki mpira: PSV 53%, Arsenal 47%
-Pasi zote: PSV 445, Arsenal 400
-Pasi sahihi: PSV 365, Arsenal 330
-Kucheza faulo: PSV 9, Arsenal 10
-Kupiga kona: PSV 5, Arsenal 3