Arsenal yatabiriwa mabaya

LONDON, ENGLAND. BEKI wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand haamini kama Arsenal itachukua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na badala yake ameipa Manchester City nafasi ya kutetea taji hilo.

Rio ametabiri timu tatu zitakazomaliza juu ya msimamo ni  Liverpool, Arsenal na Man City ambayo ndio ameipa ubingwa na inaweza kuangusha alama mbili au tatu.

Kwa mujibu wake mechi ambayo inaweza ikasababisha aangushe pointi ni dhidi ya Tottenham na inaweza kupata sare ya mabao.

Kwa upande wa Arsenal ameitoa kwenye ubingwa kwa sababu bado ina mechi ngumu zinakuja kuanzia kwa Man United, Tottenham na Chelsea.

Ferdinand anaamini washika mitutu hao watapoteza mara mbili katika mechi zao sita za mwisho hali itakayowanyima ubingwa.

Aliitabiria kupoteza mchezo wa jana dhidi ya Aston Villa kisha itapoteza mchezo na Tottenham na Manchester United zote kwa tofauti ya bao moja.

Staa huyu wa zamani wa timu ya taifa ya England pia alisema baada ya Liverpool kufunga mabao 3-0 dhidi ya Atalanta ni kama wamechanganyikiwa hivyo watawekeza nguvu kwenye Europa League kwa ajili ya kushinda mchezo wa marudiano na itapumzika siku mbili tu kisha watacheza na Fulham na baadae Everton na watapumzika siku mbili pia.

Ufinyu wa muda wa kupumzika kutoka mechi moja kwenda nyingine pamoja na nguvu ambayo wachezaji wataitumia katika mchezo wa marudiano vyote vinamuaminisha Ferdinand Liverpool pia haitotoboa.

Mchezo na Villa utakuwa mgumu kwa sababu timu hiyo inapambana kufuzu Ligi ya Mabingwa wakati ule wa Everton ni dabi yao.