Arsenal 'yamoto' EPL, Arteta asisitiza kupambana
Muktasari:
- Bao la Martin Zubimendi pamoja na mabao mawili ya mwisho kutoka kwa Viktor Gyokeres yaliiwezesha Arsenal kuongeza pengo dhidi ya Man City iliyopo nafasi ya pili kabla ya mechi za leo.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imeweka rekodi ya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi tisa kwa mara ya kwanza tangu ilipotwaa ubingwa wake wa mwisho mwaka 2004, lakini kocha wake Mikel Arteta amesisitiza kuwa pengo hilo la alama halimaanishi chochote katika mbio zao za ubingwa.
Bao la Martin Zubimendi pamoja na mabao mawili ya mwisho kutoka kwa Viktor Gyokeres yaliiwezesha Arsenal kuongeza pengo dhidi ya Man City iliyopo nafasi ya pili kabla ya mechi za leo.
Arteta, ambaye atakuwa na kibarua kingine cha kuiongoza Arsenal Alhamisi kuvaana na Brentford, amesema: "Haimaanishi chochote. Bado tunapaswa kushinda michezo mingi ili kufikia kile tunachokitaka, hivyo tusijikite huko kwenye kuamini tumeshaweza. Tumefanya kazi yetu, tumefanya kile tulichopaswa kufanya. Tutaangalia pale tulipokosea na kuboresha ili kufanya vizuri zaidi dhidi ya Brentford.”
Arsenal imekuwa kama ikipambana sana na kukaribia kuchukua ubingwa wa EPL tangu ilipofanya hivyo mwaka 2004, lakini mara kadhaa imekuwa ikishindwa na kujikuta ikimaliza nafasi ya pili katika dakika za mwisho.
Tangu mwaka 2004, imemaliza nafasi ya pili mara tano, mara tatu kati ya hizo zikiwa katika misimu mitatu iliyopita.
Arteta pia alizungumzia kiwango cha nyota wake Gyokeres ambaye alifunga mabao mawili katika mechi hiyo akisema: "Mchezaji unapojisikia kujiamini uwanjani, huwa unafanya vitu sahihi sana na hicho ndicho alichokifanya. Alionyesha kiwango cha juu.
“Sisi sote tupo nyuma yake kila wakati, tukijaribu kumsaidia na kumuunga mkono. Anatupa matokeo, na yuko katika wakati mzuri sana sasa.”
Kipigo hicho kiliendeleza matatizo ya Sunderland katika michezo ya ugenini kwenye Ligi Kuu.
The Black Cats, ambao wamekuwa wakifanya vizuri sana nyumbani msimu huu na bado ni timu pekee isiyopoteza mchezo wa Ligi Kuu ikiwa nyumbani, haijashinda mechi ya ugenini tangu Oktoba na imefunga mabao sita tu ugenini.
Kocha wa Sunderland, Regis Le Bris, amesema: "Arsenal ilikuwa bora sana katika kutumia nafasi ilizopata.
"Tulionyesha nidhamu ya mchezo na kwa maoni yangu tulifanya vizuri. Tulipata nafasi lakini hatukufunga. Bado sisi ni timu iliyopanda daraja hivi karibuni na tunaendelea kufanya vizuri. Tulikuwa washindani katika mchezo huo. Ubora wa kikosi chao ni tofauti na wetu hasa upande wa pembeni walikuwa na wachezaji wabunifu na waliokuwa wanaweza kuleta utofauti."