Arsenal kazi ipo, mechi tatu siku saba
Muktasari:
- The Gunners ilijihakikisha nafasi katika fainali baada ya kuifunga Chelsea 1-0 na hivyo kushinda jumla ya mabao 4-2 dhidi ya wapinzani wao wa jijini London.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL italazimika kucheza mechi tatu ndani ya siku saba kabla ya dabi muhimu ya Kaskazini mwa London, baada ya kufuzu fainali ya Kombe la Carabao.
The Gunners ilijihakikisha nafasi katika fainali baada ya kuifunga Chelsea 1-0 na hivyo kushinda jumla ya mabao 4-2 dhidi ya wapinzani wao wa jijini London. Kikosi cha Mikel Arteta kitacheza katika Uwanja wa Wembley Machi 22, wakisaka taji lao la kwanza la msimu huu.
Hata hivyo, ratiba hiyo ya fainali imesababisha matatizo kwa upande mwingine wa Arsenal, kwani mabadiliko ya ratiba sasa yamewapa kalenda ngumu kuelekea dabi muhimu ya Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham.
Arsenal walipangwa kusafiri kucheza na Wolves, Machi 21 saa 9 alasiri, lakini mechi hiyo sasa imehamishwa hadi Februari 18 ili kutoa nafasi kwa fainali ya Kombe la Carabao.
Hii inamaanisha kuwa wachezaji wa Arteta watapitia kipindi kigumu sana kabla ya kwenda kukabiliana na wapinzani wao wakubwa Spurs, Februari 22.
Kwanza watasafiri kwenda Brentford, Februari 12, kisha kuwakaribisha Wigan siku tatu baadaye, kabla ya kusafiri hadi Molineux kwa mechi ya saa 2 usiku dhidi ya Wolves, Februari 18. Arsenal itakuwa na siku tatu tu za kupumzika baada ya msururu huo mgumu wa mechi kabla ya kucheza ugenini kwa Spurs.
Kwa upande mwingine, Spurs watakuwa na mapumziko ya siku 12 kabla ya dabi hiyo, huku mechi ya mwisho kabla ya hapo ikiwa dhidi ya Newcastle Februari 10.
Arteta tayari ameiomba Ligi Kuu England kuongeza idadi ya wachezaji wanaoruhusiwa katika kikosi cha siku ya mechi ili kumruhusu kufanya mabadiliko zaidi. Amesema: “Natamani msimu ujao Ligi Kuu iruhusu wachezaji 20 wa uwanjani (kwenye kikosi cha mechi), badala ya 18. Nawaomba sana.”