Arsenal yakoleza moto kwa Gyokeres

Muktasari:
- Mawakala wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden walikutana na wamiliki wa Arsenal ili kufanya biashara, huku mpango wa kutimkia Manchester United ukiwa haujafungwa.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imeripotiwa kukoleza moto kunasa saini ya straika Viktor Gyokeres kutoka Sporting CP kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Mawakala wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden walikutana na wamiliki wa Arsenal ili kufanya biashara, huku mpango wa kutimkia Manchester United ukiwa haujafungwa.
Gyokeres aling’ara na kikosi cha Sporting kwa misimu miwili iliyopita na amefunga karibu mara mbili zaidi ya wachezaji wengine kwenye Primeira Liga msimu uliopita. Straika huyo ni mmoja kati ya mastaa wawili wanaosakwa na Arsenal kwa nguvu zote, sambamba na fowadi wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, wakati huu kocha Mikel Arteta akitaka kuboresha safu ya ushambuliaji ili kubeba taji la Ligi Kuu England baada ya kumaliza nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo.
Arsenal itampa nafasi straika huyo wa zamani wa Coventry City kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, kitu ambacho wapinzani wao kwenye mbio za kumsaka, Man United haitaweza kumpa huku ikitegemea ushawishi wa kocha Ruben Amorim, ambaye alimnoa staa huyo huko Sporting.
Na sasa kwa mujibu wa gazeti la Record la Ureno, wakala wa Gyokeres, Hasan Cetinkaya alikutana na wamiliki wa Arsenal. Kwa mujibu wa gazeti hilo imedaiwa majadiliano yalikuwa ishu ya biashara ya mchezaji huyo.
Na ripoti hizo zilifichua kwamba Man United bado ipo kwenye dhamira ya wazi ya kunasa saini ya mchezaji huyo kutokana na kuwasiliana na mawakala wa Gyokeres.
Nyota huyo amekuwa akisakwa na timu za Ulaya baada ya kufunga mabao 54 katika mechi 52 alizocheza msimu huu, huku kipengele kinachobainisha bei anayouzwa ni zaidi ya Pauni 60 milioni.