Arsenal, Liverpool vita nzito kumpigania Rodrygo Madrid
Muktasari:
- Rodrygo, ambaye msimu uliopita alifunga mabao 14 na kutoa asisti 11 amekuwa akihusishwa kuondoka Madrid kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza na hana furaha katika timu hiyo.
LIVERPOOL na Arsenal zinajiandaa kutuma ofa Real Madrid dirisha la usajili la Januari kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo na Brazil, Rodrygo, 24.
Rodrygo, ambaye msimu uliopita alifunga mabao 14 na kutoa asisti 11 amekuwa akihusishwa kuondoka Madrid kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza na hana furaha katika timu hiyo.
Madrid ipo tayari kumuuza Rodrigo lakini inahitaji kiasi kisichopungua Euro 100 milioni.
Mabosi wa Liverpool wanamwona fundi huyu kama mbadala wa muda mrefu wa Mohamed Salah ambaye anatarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu kwenda Saudi Arabia.
Arsenal wanavutiwa na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi za eneo la ushambuliaji, lakini kwao changamoto inaonekana kuwa ni kiasi cha pesa kinachohitajika na Madrid.
Timu nyingi zinaonekana kuwa tayari kulipa chini ya Euro 70 milioni ili kumnunua staa huyu, zikiona Euro 100 milioni ni kiasi kikubwa cha pesa, lakini bado Madrid imeendelea kushikilia msimamo wa kuhitaji kiasi hicho.
Mohamed Salah
TIMU za Ligi Kuu Saudi Arabia zinaendelea kumfuatilia mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah, 33, ambaye kwa sasa anaonekana kutokuwa na furaha kikosi cha majogoo hao.
Salah anawindwa sana na klabu kama Al-Ittihad, Al-Hilal na Al-Ahli, ambazo zipo tayari kulipa Pauni 150 milioni ili kumnunua.
Mkataba wa Liverpool na Salah unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu huu amecheza mechi 18 za michuano yote na kufunga mabao matano.
Marc Guehi
LIVEPPOOL imefungua tena mazungumzo na mawakala wa beki wa Crystal Palace na England Marc Guehi, 25, wanayehitaji kujaribu kumsajili katika dirisha la usajili la Januari baada ya kufeli kumpata katika dirisha lililopita.
Mkataba wa sasa wa Guehi unamalizika mwisho wa msimu huu na Liverpool inamwangalia kama mbadala wa Ibrahim Konate ambaye pia mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu lakini amegoma kusaini akidaiwa ana mpango wa kutimka.
Christos Mouzakitis
MANCHESTER United inafuatilia kiungo kijana wa Olympiacos na timu ya taifa ya Ugiriki Christos Mouzakitis, ambaye Real Madrid nayo inamnyemelea kimya kimya ikiwa tayari kutoa hadi Pauni 25 milioni kwa ajili ya kinda huyo mwenye umri wa miaka 18.
Mouzakitis amekuwa gumzo Ulaya kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi ndefu, kumiliki mpira na kutengeneza mashambulizi.
Amecheza mechi 14 msimu huu akiwa na mabao matatu na kutoa asisti tano.
Marcus Rashford
BARCELONA bado haijafanya uamuzi wa mwisho juu ya kumsainisha mkataba wa moja kwa moja mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford, 28, ambaye yuko kwa mkopo katika kikosi chao.
Rashford ameonekana kurejea kwenye ubora wake, akifunga mabao manne na kutoa asisti mbili katika mechi 11 za ligi hiyo. Kutokufanya uamuzi kwa Barca kunasababishwa na hali yao ya kiuchumi.
Tiago Gabriel
WEST Ham United na Brentford zinajiandaa kuwasilisha ofa dirisha la usajili la Januari kwa ajili ya beki wa kati wa Lecce, Tiago Gabriel, 20, lakini zinakumbana na ushindani mkali kutoka Juventus.
Mkataba wa sasa wa Gabriel unamalizika 2027, lakini kuna kipengele kinachowezesha Lecce na wawakilishi wa staa huyo kuurefusha kwa miaka miwili zaidi kwa makubaliano. Msimu huu amecheza mechi 15 za michuano yote.
Guglielmo Vicario
KIPA wa Tottenham Hotspurs, Guglielmo Vicario, 29, anafikiria kuondoka dirisha lijalo la majira ya baridi kurudi Italia ambako Inter Milan inahitaji huduma yake.
Vicario amecheza mechi 14 za Ligu Kuu England msimu huu na amemaliza nne kati ya hizo bila ya kuruhusu bao.
Inter inamwona kama mrithi sahihi wa muda mrefu wa Yann Sommer, hasa baada ya kuonyesha kiwango kizuri.
Ederson
LIVERPOOL imepiga hatua kubwa katika mchakato wa kuiwania saini ya kiungo wa Atalanta na Brazil, Ederson, 26, dirisha lijalo la majira ya baridi.
Mbali ya Liverpool, huduma ya Ederson pia inahitajika na Barcelona ambayo inaonekana kusuasua kutokana na hali yao ya kiuchumi.
Ederson amekuwa kwenye kiwango bora sana Serie A tangu msimu uliopita. Mkataba unamalizika mwaka 2027.