Prime
Arsenal kwenye mitindo minne ya kijanja kuizima Real Madrid

Muktasari:
- Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta inakabiliwa na kasheshe la kukosa wachezaji wanne muhimu kwenye safu yake ya ulinzi, huku mbele yao wakikabiliwa na mechi ngumu kabisa ya robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, Jumanne, Aprili 8 uwanjani Emirates.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imejikuta kwenye janga jingine la majeruhi kwenye kikosi na bahati mbaya pengine jambo hilo limetokea kwenye kipindi kibaya zaidi.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta inakabiliwa na kasheshe la kukosa wachezaji wanne muhimu kwenye safu yake ya ulinzi, huku mbele yao wakikabiliwa na mechi ngumu kabisa ya robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, Jumanne, Aprili 8 uwanjani Emirates.
Beki wa kati Gabriel alitolewa uwanjani dakika ya 16 katika mchezo wa ushindi wa mabao 2-1 iliyopata Arsenal dhidi ya Fulham kwenye Ligi Kuu England, Jumanne iliyopita na Mbrazili huyo atahitaji kufanyiwa upasuaji kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli ya paja.
Beki wa kulia, Jurrien Timber naye yupo kwenye hatihati kubwa ya kuwakabili Los Blancos kutokana na kupata maumivu ya goti kwenye mechi dhidi ya Fulham na alishindwa kumaliza na kutolewa.
Mabeki hao wawili, wanaungana na wengine wawili Ben White na Riccardo Calafiori, ambao pia wamekuwa nje ya uwanja kwa muda, wakihitaji tiba kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti.
Wakati White akikimbizana na muda ili kuwa fiti acheze kwenye mechi ya Everton itakayofanyika Jumamosi hii, Calafiori hali yake bado haipo vizuri, ataendelea kuwa nje ya uwanja baada ya kuumia alipokuwa na timu ya taifa ya Italia.
Jambo hilo linamfanya kocha Arteta kichwa kumpasuka kwelikweli akiwaza namna atakavyoanza na safu yake ya ulinzi kwenye mechi ngumu dhidhi ya kikosi cha Galacticos cha Carlo Ancelotti.
Hata hivyo, mechi ni lazima ichezwe na hizi hapa njia kadhaa ambazo Arteta anaweza kuzitumia kwenye kukipanga kikosi chake katika kipute hicho cha kibabe dhidi ya Real Madrid.

- Partey acheze beki wa kulia
Kama White na Timber watashindwa kucheza, kocha Arteta anaweza kurudi kwa Thomas Partey - kiungo ambaye kuna nyakati alitumika sana kucheza kwenye beki ya kulia mwanzoni mwa msimu huu baada ya kutokea majeruhi kikosini.
Arsenal haina wasiwasi Partey anapocheza upande wa kulia na alipangwa kwenye eneo hilo katika mechi ngumu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati ilipoichapa AS Monaco 3-0 katika kipindi cha makundi yaliyochezwa kwa mfumo wa ligi.
Lakini, kwenye huo upande wa kulia, kasheshe atakalokutana nalo Partey ni kumkaba fowadi msumbufu wa Kibrazili, Vinicius Jr. Bila shaka, Partey atakuwa kwenye mwendo kwa dakika zote 90 kukimbizana na Mbrazili huyo.

2. Timber akipona na kupewa nafasi
Endapo Timber akionyesha kuwa na nafuu kiasi, bila shaka kocha Arteta atachagua kuanza na beki huyo kwenye upande wa kulia, lakini wasiwasi ni kwamba huenda akaenda kuumia zaidi goti lake tofauti na ilivyokuwa dhidi ya Fulham.
Timber ni mzuri kwenye kukaba na amekuwa akipanda sana mbele, jambo ambalo litakuwa chaguo bora kwa Arsenal, hasa inapokuw ana kazi ya kumdhibiti Vinicius Jr.
Kitu kizuri kwa Arsenal ni kama Timber ataanza kwenye beki ya kulia, hilo litamfanya Partey kuingia kwenye sehemu ya kiungo.
Lakini, ishu itakuwa upande mwingine, Lewis-Skelly hajawahi kucheza na Kiwior, hivyo kutakuwa na balaa zito la kumzuia Rodrygo na Kylian Mbappe.

- White arudi kucheza beki wa kati
Kama White atafiti vipimo vya ufiti, kocha Arteta basi anaweza kushawishika kumtumia staa huyo wa zamani wa Brighton na Leeds United kucheza kwenye beki ya kati.
Beki White ana uwezo mkubwa sana wa kupiga pasi, kasi na nguvu, hivyo kucheza beki wa kati halitakuwa tatizo kwake, alionyesha hilo kwenye mechi ya mabao 2-2 dhidi ya Liverpool, Oktoba mwaka jana, alipocheza sambamba na Gabriel.
Endapo kama White atacheza kwenye beki ya kati, Kocha Arteta anaweza kumtumia kwenye upande wa kushoto wa beki wa kati, akicheza sambamba na Saliba katika kuhakikisha ukuta wa miamba hiyo ya Emirates unakuwa kwenye ubora mkubwa.

- Mtindo wa kibabe zaidi
Hii inaweza kuwa hatari kujaribu, lakini inavutia na pengine ikamfanya Arteta kuonyesha ufundi wake mkubwa kama kocha, akijaribu kukibadili kikosi chake na kuiga vile mwalimu wake Pep Guardiola amekuwa akifanya kwenye mechi kubwa za aina hii.
Arteta anaweza kubadilisha mtindo wake wa uchezaji, kutoka kwenye kutumia mabeki wanne na kutumia mtindo wa 3-4-3, wakitumia mabeki wa kati watatu, wing-back wawili ili kumeza kasi yote ya mashambulizi ya Real Madrid, kwa sababu timu itakuwa na wachezaji watano wenye uwezo wa kukaba wanaposhambuliwa, pamoja na kiungo mkabaji, anayeongeza nafasi ya kuwa na watu sita kwenye eneo la kujilinda, huku ikifanya kikosi kuwa na wigo mpana wa kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Lewis-Skelly na Timber watacheza wing-back huku wachezaji Bukayo Saka na Gabriel Martinelli watatanua uwanja, kutoa nafasi ya Martin Odegaard na Mikel Merino wakitawala sehemu ya kati, huku Declan Rice akicheza kwenye kiungo ya kukaba.