Arsenal kumjaza mabilioni Arteta
Muktasari:
- Mhispania huyo aliiongoza Arsenal kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa ligi baada ya miaka 22 msimu huu, huku ushindi huo ukithibitishwa Jumanne usiku baada ya Manchester City kushindwa kuifunga AFC Bournemouth.
LONDON, ENGLAND: Kocha wa Mabingwa wa ligi Kuu England, Mikel Arteta yuko mbioni kuwa mmoja wa makocha wanaolipwa zaidi duniani wakati wa akijiandaa kusaini mkataba mpya na Arsenal.
Mhispania huyo aliiongoza Arsenal kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa ligi baada ya miaka 22 msimu huu, huku ushindi huo ukithibitishwa Jumanne usiku baada ya Manchester City kushindwa kuifunga AFC Bournemouth.
Mkataba wa sasa wa Arteta ulikuwa unatarajiwa kumalizika majira ya kiangazi ya mwaka ujao, lakini mazungumzo ya kuongeza mkataba huo yako katika hatua za mwisho.
Makubaliano hayo mapya yanatarajiwa kumpa nyongeza kubwa ya mshahara, hatua ambayo itamweka miongoni mwa makocha wanaoingiza fedha nyingi zaidi katika soka la dunia.
Hii ni zawadi ya mafanikio makubwa aliyoyaleta klabuni tangu achukue mikoba mwaka 2019, baada ya kuijenga upya Arsenal kutoka kipindi kigumu hadi kuwa mabingwa wa England tena.
Kwa mafanikio haya, Arteta ameonyesha kuwa uvumilivu wa klabu na kauli yake ya “amini mchakato” ilikuwa na maana halisi na sasa analipwa kwa matokeo yake.
Diego Simeone anaaminika ndiye kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani kwa sasa, akipokea takribani pauni26 milioni kwa mwaka akiwa na Atletico Madrid.
Kwa sasa, Arteta analipwa takribani pauni10 milioni 10 kwa mwaka, pamoja na bonasi ya pauni5 milioni kwa kuifikisha Arsenal kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa UEFA.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, mkataba wake mpya utamletea ongezeko kubwa la kipato na kumuweka kwenye kundi la makocha wanaolipwa zaidi katika soka la dunia.
Kwa kulinganisha, Pep Guardiola analipwa karibu pauni20 milioni kwa mwaka akiwa na Manchester City.
Pia, baada ya Guardiola kuondoka City majira haya ya kiangazi, Arteta atachukua rasmi nafasi ya kuwa kocha aliyekaa muda mrefu zaidi ndani ya klabu ya Ligi Kuu England.
Hiyo ni hatua nyingine kubwa katika safari yake ya ukocha kutoka kuwa msaidizi wa Guardiola akiwa City, hadi kuwa mmoja wa makocha wenye ushawishi mkubwa na wanaolipwa zaidi duniani baada ya kuirejesha Arsenal kileleni mwa soka la England.
Mazungumzo yanatarajiwa kuendelea tena baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa UEFA mwishoni mwa wiki ijayo.
Wakati huo huo, kocha wa Arsenal, Arteta, pia anaelekeza nguvu zake katika kumsajili mshambuliaji chipukizi wa AFC Bournemouth, Eli Junior Kroupi, katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi huku akitaka kuimarisha kikosi chake zaidi.
Kroupi ndiye aliyefunga bao lililoihakikishia Arsenal ubingwa baada ya Bournemouth kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Manchester City Jumanne usiku.
Inaaminika Bournemouth watahitaji kiasi cha pauni 80 milioni ili kumwachia nyota huyo.
Mchezaji huyo mwenye miaka 19 ameweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi kwa kijana wa umri huo katika msimu wake wa kwanza ndani ya Ligi Kuu, akifikisha mabao 13 baada ya kuifunga Man City.
Pia ameripotiwa kubadili wakala wake kuelekea dirisha la usajili la majira ya kiangazi, ishara inayoongeza uvumi kuhusu uwezekano wa kuhamia klabu kubwa.
Inaaminika pia kwamba Arsenal wameandaa fedha za kutosha kumruhusu Arteta kufanya usajili mkubwa wa nyota wa kiwango cha juu katika dirisha lijalo.