Arsenal na miaka 22 ya kusubiri ubingwa wa EPL
Muktasari:
- Arsenal sasa imefanikisha ndoto ya kusubiriwa kwa miaka 22 baada ya kuwa mabingwa wa England tena.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya miaka mingi ya kukaribia mafanikio bila kuyafikia, hatimaye Arsenal imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2025-2026. Ni ubingwa uliotokana na uimara mkubwa wa safu ya ulinzi na matumizi mazuri ya nafasi zilizopatikana kufunga mabao.
Arsenal sasa imefanikisha ndoto ya kusubiriwa kwa miaka 22 baada ya kuwa mabingwa wa England tena.
Sare ya bao 1-1 ya Manchester City dhidi ya Bournemouth, Jumanne usiku wa Mei 19, 2026, imeihakikishia Arsenal ubingwa huo kutokana na kuweka pengo la pointi nne lisilofikiwa na mpinzani yeyote ndani ya ligi hiyo ikibaki mechi moja kwa kila timu.
Huu ni ubingwa wao wa 14 wa Ligi Kuu England, wa nne tangu kuanzishwa kwa Premier League 1992, na wa kwanza tangu kikosi maarufu cha Invincibles cha msimu wa 2003-2004.
Ikiwa msimu ule wa kutopoteza mchezo hata mmoja ulitambulika kwa namba sifuri (0), basi huu wa 2025-2026 umetawaliwa na takwimu mbalimbali zilizofafanua safari yao ya ubingwa.
Tayari ratiba ya gwaride la kusherehekea ubingwa huo imetoka ambapo litafanyika Jumapili ya Mei 31, 2026, siku moja baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain mjini Budapest.
Mipango ya awali inaonyesha kuwa basi litaanzia safari yake kutoka Uwanja wa Emirates kupitia maeneo ya Drayton Park, Aubert Park, Highbury Grove, St Paul’s Road na Upper Street kabla ya kurejea tena uwanjani hapo.
Sababu ya gwaride hilo kufanyika Mei 31, 2026 ni kwamba baadhi ya nyota wa Arsenal wanaotarajiwa kushiriki Kombe la Dunia 2026 wanapaswa kujiunga na timu zao za taifa kuanzia Jumatatu ya Juni 1, 2026.
Mashabiki watakaosafiri kwenda Budapest kwa ajili ya fainali hiyo ya UEFA watapaswa kurejea haraka London ili wasikose shamrashamra hizo kubwa za kihistoria.
Iwapo Arsenal itaifunga PSG katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mei 30, 2026 huko Puskás Aréna, basi itasherehekea mataji yote mawili kwenye gwaride hilo la basi la wazi. Endapo itashindwa, gwaride bado litafanyika kwa ajili ya kusherehekea taji la Premier League pekee.
MABAO YA KONA (18)
Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal imeendelea kujulikana kwa ubora wake kwenye mipira ya adhabu na kona.
Msimu huu, timu hiyo imefunga mabao 28 kati ya 68 ya ligi kupitia mipira iliyokufa, ikiwa ni mabao matatu zaidi ya timu yoyote nyingine.
Hata hivyo, kona zimekuwa silaha yao kubwa zaidi baada ya kufunga mabao 18 kupitia mazingira hayo, rekodi mpya katika historia ya Premier League kwa msimu mmoja.
Rekodi ya awali ilikuwa mabao 16 yaliyofungwa na Oldham Athletic msimu wa 1992-1993. Arsenal ilivunja rekodi hiyo kabla ya Tottenham kufikisha mabao 17 ya kona msimu huu.
Ingawa baadhi ya wakosoaji wamekuwa wakisema utegemezi wa mipira ya adhabu unaifanya Arsenal kuwa timu inayotabirika, ukweli ni kwamba timu kubwa duniani zimekuwa zikifaidika kwa kutumia vizuri nafasi ndogo kama hizi. Arsenal imekuwa bora kuliko wote katika eneo hili.
CLEAN SHEETS ZA DAVID RAYA (19)
Mlinda mlango David Raya ameonyesha kiwango bora msimu huu baada ya kufikisha michezo 19 bila kuruhusu bao.
Hii imemfanya alingane na rekodi ya makipa wa Arsenal waliowahi kuwa na clean sheets nyingi zaidi ndani ya msimu mmoja wa Premier League, akimfikia David Seaman aliyefanya hivyo misimu ya 1993-1994 na 1998-1999.
Iwapo Raya atamaliza bila kuruhusu bao katika mchezo wa mwisho dhidi ya Crystal Palace, ataweka rekodi mpya ya klabu.
Pia ameshinda tuzo ya Golden Glove kwa msimu wa tatu mfululizo, akijiunga na orodha ya makipa wachache waliowahi kufanya hivyo akiwemo Pepe Reina, Joe Hart na Ederson.
WASTANI WA KURUHUSU BAO KWA MECHI (0.74)
Ubingwa wa Arsenal umejengwa zaidi kwenye uimara wa safu ya ulinzi.
Timu hiyo imeruhusu mabao 26 pekee katika ligi msimu huu, idadi ndogo zaidi kulinganisha na timu nyingine zote, na ya pili kwa ubora katika historia ya Arsenal kwenye Premier League baada ya msimu wa 1998-1999 walioruhusu mabao 17.
Kwa mujibu wa takwimu za wastani wa kuruhusu bao kwa mechi (xGA), Arsenal imeruhusu wastani wa mabao 0.74 kwa kila mchezo, moja ya rekodi bora zaidi tangu takwimu hizi zilipoanza kufuatiliwa mwaka 2012.
Aidha, imekuwa ikipewa wastani wa mashuti 8.2 kwa mechi na mashuti 2.4 yaliyolenga lango, ikiwa timu bora zaidi katika ligi tano kubwa Ulaya.
USHINDI WAKATI GABRIEL NA SALIBA WAKIANZA PAMOJA (17)
Msingi wa uimara wa ulinzi wa Arsenal umetokana na ushirikiano wa mabeki wa kati William Saliba na Gabriel Magalhães.
Wawili hao wameanza pamoja mechi 26 za ligi msimu huu, huku Arsenal ikishinda michezo 17, idadi inayolingana na pacha bora zaidi kwenye ligi.
Zaidi ya hayo, Arsenal imepata clean sheet 15 katika mechi hizo 26, ikiwa ni wastani wa mchezo mmoja bila kufungwa bao kila mechi 1.7.
POINTI DHIDI YA TIMU ZA NUSU YA CHINI (53)
Katika misimu iliyopita, Arsenal mara nyingi ilionekana kushindana vizuri dhidi ya timu kubwa lakini kupoteza pointi muhimu kwa timu ndogo. Safari hii mambo yalibadilika.
Arsenal imeshinda mechi 17 kati ya 19 dhidi ya timu zinazoshika nafasi za nusu ya chini ya msimamo, ikikusanya pointi 53 na kuruhusu mabao sita pekee.
Wamekuwa na wastani wa pointi 2.8 kwa kila mechi dhidi ya timu hizo, kiwango kinachowazidi hata Manchester City iliyokuwa na wastani wa pointi 2.3.
SIKU ILIZOKAA KILELENI (238)
Arsenal imekuwa ikipewa lawama kwa kushindwa kumalizia kazi baada ya kuongoza ligi kwa muda mrefu katika misimu ya karibuni. Lakini safari hii imekuwa tofauti.
Mwisho wa msimu huu, Arsenal itakuwa imeongoza msimamo wa ligi kwa siku 238, zaidi kwa siku 204 ukilinganisha na Liverpool na siku 229 zaidi ya Manchester City.
Msimu wa 2022-2023 waliongoza kwa siku 232 lakini wakashindwa kubeba ubingwa. Safari hii hawakurudia makosa hayo.
MABAO YA VIKTOR GYÖKERES (14)
Viktor Gyökeres aliyetua mwanzoni mwa msimu huu, amekuwa na mchango mkubwa licha ya Arsenal kutegemea zaidi uimara wa ulinzi. Mshambuliaji huyo amefunga mabao 21 katika mashindano yote na 14 kwenye Premier League.
Amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 20 au zaidi katika msimu wake wa kwanza Arsenal tangu Alexis Sánchez alivyofanya hivyo msimu wa 2014-2015.
Cha kushangaza, mabao 14 ni kiwango kidogo kwa mfungaji bora wa timu bingwa wa Premier League, yakilingana na rekodi ya Eric Cantona msimu wa 1995-1996.
USHINDI WA BAO 1-0 (8)
Arsenal imeshinda kwa matokeo ya bao 1-0 mara nane msimu huu, idadi kubwa zaidi tangu msimu wa 1998-1999 ilipofanya hivyo mara tisa.
Katika kipindi cha mwisho cha mbio za ubingwa, ushindi wa mabao 1-0 umekuwa silaha muhimu ya timu hiyo huku ikionyesha ukomavu mkubwa wa kulinda matokeo.
MECHI WALIZOPITWA KWA KUKIMBIA (2)
Chini ya Arteta, Arsenal imejengwa kwa msingi wa nguvu, stamina na uwezo wa kimwili. Cha kushangaza, Arsenal imekimbia umbali mkubwa kuliko wapinzani wao katika mechi 35 kati ya 37 za ligi msimu huu, zaidi ya timu yoyote England.
Hata kwa wastani wa kumiliki mpira wa asilimia 56.1, timu hiyo bado imekuwa na kiwango kikubwa cha kazi uwanjani, ikiongozwa na nyota kama Declan Rice.
UMRI WA ARTETA (MIAKA 44 NA SIKU 54)
Mwisho kabisa, mafanikio haya hayawezi kutenganishwa na kazi ya Arteta. Akiwa na miaka 44 na siku 54, Arteta anakuwa kocha wa pili mwenye umri mdogo zaidi kushinda Premier League, nyuma ya José Mourinho aliyefanya hivyo akiwa na miaka 42.
Baada ya zaidi ya miaka sita akiwa Arsenal, huku Pep Guardiola akitarajiwa kuondoka Manchester City mwishoni mwa msimu, Arteta sasa anakuwa mmoja wa makocha wenye muda mrefu zaidi ndani ya Premier League.
Kwa namna alivyoijenga Arsenal taratibu hadi kufikia mafanikio haya, wapinzani wao wana sababu ya kuwa na wasiwasi, huenda huu ukawa mwanzo wa enzi mpya ya mafanikio kwa miamba hiyo ya London Kaskazini.
MSIMU NAFASI
2025–26: 1
2024–25: 2
2023–24: 2
2022–23: 2
2021–22: 5
2020–21: 8
2019–20: 8
2018–19: 5
2017–18: 6
2016–17: 5
2015–16: 2
2014–15: 3
2013–14: 4
2012–13: 4
2011–12: 3
2010–11: 4
2009–10: 3
2008–09: 4
2007–08: 3
2006–07: 4
2005–06: 4
2004–05: 2
MAKOCHA WALIOPITA
Unai Emery (Mei 2018 – Novemba 2019): Aliteuliwa kuwa mrithi wa moja kwa moja wa Arsène Wenger, akisimamia mechi 78 za Arsenal. Aliiongoza timu kufika fainali ya Kombe la UEFA Europa League mwaka 2019 kabla ya kuondoshwa baada ya mwanzo mgumu wa msimu uliofuata.
Freddie Ljungberg (Kocha wa muda, Novemba 2019 – Desemba 2019): Kiungo wa zamani wa Arsenal na mmoja wa magwiji wa klabu hiyo, alipewa jukumu la kuinoa timu ya kwanza kwa muda, akisimamia mechi sita kabla ya kupatikana kwa kocha wa kudumu.
Mikel Arteta (Desemba 2019 – sasa): Nahodha wa zamani wa Arsenal, alirejea klabuni kama kocha mkuu. Aliijenga upya timu, akairudisha kwenye ushindani wa juu wa soka la England na hatimaye ameipa ubingwa wa Ligi Kuu England.