Ticha, mwanafunzi kuonyeshana ubabe
Muktasari:
- Cha kushangaza, hiyo ilikuwa mara ya mwisho Guardiola kumshinda Arteta, tangu wakati huo, inaonekana Arteta ndiye mwenye ujanja wa kumdhibiti mwalimu wake.
MANCHESTER, ENGLAND: ARSENAL na Manchester City zitakutana katika fainali ya Kombe la Ligi mwezi ujao, pambano litakalomkutanisha mwanafunzi Mikel Arteta dhidi ya mwalimu wake Pep Guardiola.
Arteta, 43, aliwahi kuwa msaidizi wa Guardiola katika kikosi cha Man City kwa miaka mitatu kabla ya kuchukua nafasi ya ukocha mkuu wa Arsenal 2019. Wawili hao walishinda mataji kadhaa ikiwemo Kombe la Ligi 2018, wakiiangusha Arsenal katika mashindano hayo.
Guardiola aliendelea kushinda mataji mengi baada ya Arteta kuondoka Etihad, akimzidi hata aliyekuwa msaidizi wake katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England 2023 na 2024.
Hata hivyo, pengo kati yao limekuwa likipungua katika miaka ya hivi karibuni. Arsenal ilifanikiwa kumaliza juu ya Man City msimu uliopita, japokuwa bado walikuwa nyuma ya Liverpool na kwa sasa wanawaongoza Man City kwa pointi sita katika mbio za ubingwa wa msimu huu.
Arteta aliweza kupata ushindi mkubwa mapema katika taaluma yake ya ukocha dhidi ya Guardiola, akimshinda 2-0 katika nusu fainali ya Kombe la FA mwaka 2020, mechi iliyochezwa bila mashabiki, baada ya kutumia mfumo wa mabeki watatu.
Arsenal ilifanikiwa kushinda Kombe la FA msimu huo, likiwa taji la kwanza kwa Arteta kama kocha mkuu.
Hata hivyo, ushindi wa nusu fainali ungekuwa pekee dhidi ya Guardiola katika mechi tisa ya kwanza, huku Arsenal ikipoteza mara nane zilizobaki.
Miongoni mwa vipigo hivyo ni pamoja na cha 5-0 ilichopata Etihad, Agosti 2021, na kupigo cha 4-1 Aprili 2023, matokeo yaliyozima ndoto ya Arsenal ya ubingwa msimu huo.
Cha kushangaza, hiyo ilikuwa mara ya mwisho Guardiola kumshinda Arteta, tangu wakati huo, inaonekana Arteta ndiye mwenye ujanja wa kumdhibiti mwalimu wake.
Makocha hao wawili wamekutana mara sita tangu hapo, Arsenal ikishinda mechi tatu huku tatu nyingine zikiisha kwa sare.