Arsenal inaongoza ligi VAR ikifutwa 2024-25

Muktasari:
- Licha ya kushinda 5-1 dhidi ya Manchester City, kikosi hicho cha Kocha Mikel Arteta bado kimeachwa pointi sita na Liverpool kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku miamba hiyo ya Anfield ikiwa na mchezo mmoja mkononi.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Arsenal ingekuwa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England endapo kama kusingekuwa na VAR.
Licha ya kushinda 5-1 dhidi ya Manchester City, kikosi hicho cha Kocha Mikel Arteta bado kimeachwa pointi sita na Liverpool kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku miamba hiyo ya Anfield ikiwa na mchezo mmoja mkononi.
Lakini, kama mechi zingekuwa zinaamriwa na waamuzi wa uwanjani tu na si wale wanaotumia msaada wa picha za video (VAR), basi Arsenal ingekuwa na pointi sita zaidi, wakati Liverpool ingekuwa na pointi pungufu na ilizonazo kwa sasa.
Jambo hilo lingeifanya Arsenal kushika usukani wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Liverpool. Arsenal ilikuwa na matukio matano tu ya VAR yaliyoingilia kubadilisha matokeo yao katika mechi 24 ilizocheza kwenye ligi. Moja ya tukio hilo ni lile bao la dakika za majeruhi la Kai Havertz kwenye ushindi wa 4-2 dhidi ya Leicester City, ambalo ilionekana kama mchezaji ameotea kabla ya VAR kuwapa faida wakali hao wa Arteta.
Matukio mengine ni la kadi ya njano ya William Saliba wakati alipomchezea rafu straika wa Bournemouth, Evanilson akiwa mtu wa mwisho na hata hivyo, mechi hiyo ilimalizika kwa Arsenal kukubali kichapo cha mabao 2-0. Lakini, matukio mengine matatu, ambayo yote yalionekana kuwa sahihi, yaliinyima ushindi Arsenal. Havertz alidhani amefunga kuipa uongozi timu yake kwenye kipindi cha kwanza baada ya sare ya 1-1 na Chelsea, lakini VAR ilifuta bao hilo.
Kisha lile tulio la kuotea Gabriel Martinelli kwenye mechi la dakika 88 la Bukayo Saka, ambalo lingekuwa la ushindi dhidi ya Fulham. VAR pia iliingilia matokeo ya bao la dakika za mwisho la Mikel Merino kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Aston Villa.
Liverpool ilibebwa kwa bao lao la pili kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Manchester United baada ya VAR kudai mchezaji Matthijs de Ligt alishika mpira kwenye boksi na kumpa ruhusa ya Mohamed Salah kufunga kwa mkwaju wa penalti. Uamuzi huo wa VAR haukuwa sahihi, lakini Liverpool iliwanufaika.
Bila ya VAR, Bournemouth ingekuwa kwenye nafasi ya nne katika msimamo na PGMOL ilikiri bao lao la ushindi dhidi ya Newcastle United lilikataliwa kimakosa na VAR kwa madai mchezaji Dango Ouattara ameshika mpira.
Newcastle kwa upande wao wamekuwa na matukio 10 ya VAR yaliyokwenda vizuri upande wao, huku mawili tu ndiyo yaliyowabana wao, huku teknolojia hiyo ya kutumia mwamuzi wa video kuigharimu Man United pointi nne.