Arrigo Sacchi amtaka Zidane atue Juventus
Muktasari:
- Alipozungumza wikiendi iliyopita kwenye tamasha la Trento Sports Festival, Zizou alisema ameacha milango kwa ajili ya kwenda kuinoa Juve. Na Sacchi amekaribisha jambo hilo akisema: "Nilijiuliza mwenyewe kwanini asiwe kocha wa kwenda kuirudisha ile mashine ifanye kazi?
TURIN, ITALIA: KOCHA wa zamani wa AC Milan, Arrigo Sacchi amefunguka kwamba anapenda kumwona Zinedine Zidane anarejea Juventus.
Alipozungumza wikiendi iliyopita kwenye tamasha la Trento Sports Festival, Zizou alisema ameacha milango kwa ajili ya kwenda kuinoa Juve. Na Sacchi amekaribisha jambo hilo akisema: "Nilijiuliza mwenyewe kwanini asiwe kocha wa kwenda kuirudisha ile mashine ifanye kazi?
"Nafahamu anataka kuwa kocha wa Ufaransa na hilo linaeleweka. Akiwa mchezaji, alikuwa shujaa wa nchi, aliongoza mapambano ya kuiteka dunia na kisha Ulaya."
Aliambia pia La Gazzetta dello Sport: "Hata hivyo, nina matumaini. Alikuwa mchezaji muhimu wa Juventus, alikuwa bingwa akivaa jezi za nyeusi na nyeupe, alikuwa na shujaa wake kama Marcello Lippi kama kocha, alijifunza mengi kutoka kwake, anafuata ushauri wake, hivyo kwanini asiwepo kwenye benchi la Juventus? Mungu anisamehe kwa sababu ningeweza kumkosea heshima (Igor) Tudor na kazi yake."
Sacchi ameongeza: "Ningempenda mtu kama Zidane, mtu anayependa soka la kushambulia, mtu anayeamini kwenye timu yake kucheza na mtu anayeruhusu vipaji, aingie kwenye dunia ya Serie A. Ligi yetu itafaidika kwa uwepo wake. Uwepo wa Zidane kwenye benchi la Juventus italeta upendo na soka la maana ambalo kwa sasa linakosekana. Hebu Zizou, fikiria juu ya hili."
Zidane katika ufundishaji wake, ameiongoza Real Madrid kwa vipindi viwili tofauti akianza Januari 4, 2016 hadi Mei 31, 2018 kisha Machi 11, 2019 hadi Mei 27, 2021, ameshinda mataji 11 ambayo ni La Liga: 2016–17 na 2019–20, Supercopa de España: 2017 na 2020, Ligi ya Mabingwa Ulaya: 2015–16, 2016–17 na 2017–18, UEFA Super Cup: 2016 na 2017, FIFA Club World Cup: 2016 na 2017.
Zidane anahesabika kama mmoja wa wachezaji mahiri kabisa wa Ufaransa kipindi cha uchezaji wake, akifunga mabao 31 katika mechi 108 za kimataifa alizochezea timu hiyo kabla ya kustaafu mwaka 2006.
Mechi yake ya mwisho Zidane alishuhudiwa akimrukia kichwa Marco Materazzi kwenye kifua katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2006, ambapo Ufaransa ilipoteza mbele ya Italia kwa mikwaju ya penalti huko Ujerumani.
Klabu alizowahi kuzichezea ni Cannes (1989–1992), Bordeaux (1992–1996), Juventus (1996–2001) na Real Madrid (2001–2006).