Arne Slot akubali kukosolewa
Muktasari:
- Mdachi huyo alirithi mikoba ya Jurgen Klopp 2024, lakini alifanikiwa kuipa Liverpool ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wake wa kwanza.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot, anakiri kuwa ni haki kupuuzia mafanikio ya msimu uliopita na kumhukumu yeye binafsi kwa misingi ya msimu wa sasa pekee, huku presha ikizidi kumkabili Mdachi huyo kwa hali ilivyo huko Anfield.
Mdachi huyo alirithi mikoba ya Jurgen Klopp 2024, lakini alifanikiwa kuipa Liverpool ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wake wa kwanza.
Hata hivyo, msimu huu mambo yamekuwa tofauti na, licha ya kuivunja rekodi ya uhamisho ya Uingereza mara mbili, klabu hiyo ya Merseyside iko hatarini kukosa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kutokana na ushindani mkali kuwania Top Four.
Licha ya kuanza kwa kasi kubwa, kiwango cha Liverpool kimeshuka kwa kasi na matatizo yao yamekuwa wazi. Kipigo dhidi ya Bournemouth katika mchezo wa mwisho kimefanya iwe michezo mitano mfululizo ya ligi bila ushindi, huku ikishika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kabla ya mechi za Jumamosi.
Matumaini ya kutetea taji yamepotea, na licha ya Slot kurejea mara kadhaa mafanikio ya msimu uliopita, sasa amekiri kuwa yuko tayari kuhukumiwa kulingana na kitakachotokea katika miezi ijayo.
Alisema: “Hilo ndilo jambo unalopaswa kulikubali ukiwa kocha ambaye hashindi mechi za kutosha. Sijui kama mtu huyo yupo hapa lakini aliniuliza swali kama mambo yamebadilika kwa makocha siku hizi. Labda hilo limebadilika kwa makocha kwamba hata umeshinda kitu bado kuna nafasi ya kukosolewa, jambo ambalo kwa kiasi fulani ni la kawaida kwa sababu tuko kwenye msimu mpya, na nilikuwa wa kwanza kuwaambia wachezaji, ‘tunahitaji kuusahau msimu uliopita.’ Nadhani ni haki kunihukumu kwa msimu huu na si kwa msimu uliopita.”
Slot amewakwaza baadhi ya mashabiki wa Liverpool karibuni na alifanya hivyo tena wiki hii baada ya kudai Liverpool ilitolewa robo fainali ya Europa League na Atalanta Aprili 2024, muda mfupi baada ya ushindi wa mabao 6–0 dhidi ya Qarabag Jumatano. Alikuwa akijaribu kuonyesha kuwa kufika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kunapaswa kuthaminiwa.