Antony kuhama Man United tu kawaka
Muktasari:
- Winga huyo aliyejiunga na Man United kwa ada ya Pauni 86 milioni akitokea Ajax mwaka 2022 alionekana mzigo na hivyo kutolewa kwa mkopo kwenda Betis dirisha la usajili la majira ya baridi mwaka huu, ambalo lilifungwa usiku wa jana Jumatatu.
MADRID, HISPANIA: YULE staa aliyeonekana kimeo kwenye kikosi cha Manchester United, Antony ameanza kwa moto kwenye timu yake anayocheza kwa mkopo, Real Betis baada ya kuhusika katika bao katika mechi yake ya kwanza tu katika kikosi hicho cha La Liga.
Winga huyo aliyejiunga na Man United kwa ada ya Pauni 86 milioni akitokea Ajax mwaka 2022 alionekana mzigo na hivyo kutolewa kwa mkopo kwenda Betis dirisha la usajili la majira ya baridi mwaka huu, ambalo lilifungwa usiku wa jana Jumatatu.
Mbrazili huyo alipokuwa Old Trafford alifunga mabao 12 na kuasisti mara tano tu katika mechi 96. Mambo yalikuwa magumu zaidi kwake msimu huu baada ya kushindwa kumshawishi kocha mpya Ruben Amorim ili kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza na ndiyo maana ametolewa kwa mkopo.
Lakini, baada ya kutua Betis, Antony amefanya kweli kwenye mechi yake ya kwanza tu, dhidi ya Athletic Bilbao uwanjani Benito Villamarin na alihitaji dakika 14 tu kusababisha bao katika mechi yake ya kwanza na kunogesha mambo kwenye timu hiyo inayonolewa na kocha Manuel Pellegrini.
Antony alipiga shuti kutoka upande wa kulia, ambalo liliokolewa na kipa wa Bilbao, Unai Simon kabla ya mpira huo kumfikia mfungaji, Isco.
Jambo hilo liliwashtua mashabiki wa Man United wakimshudia mchezaji wao akianza kwa kasi kubwa huko Hispania na kuanza kupata mashaka na timu yao kutokana na wachezaji wengi wanaoondoka kwenye timu hiyo kwenda kufanya vizuri kwingineko, wakiwamo Scott McTominay, Anthony Elanga na Jadon Sancho.
Na shabiki mmoja aliandika kwenye mtandao wa Twitter: “Antony ameanza kusababisha matatizo. Manchester United ndio tatizo.”
Mwingine aliongeza: “Anthony amehusika kwenye bao katika mechi yake ya kwanza. Pengine Manchester United ndiyo tatizo lote.”
Shabiki wa tatu alisema: “Ahhahahaha, Antony ameondoka Man U, anahusika kwenye bao. Ile klabu ni ya hovyo.”
Shabiki huyo alisema hivi: “Wachezaji wa United wanakuwa wazuri wakiondoka Man United. Antony tayari amehusika kwenye bao.”
Betis ilishindwa kushikilia uongozi wake na kujikuta ikipata sare ya mabao 2-2 katika mchezo huo juzi Jumapili.