Ancelotti, Hansi Flick kuitisha mgomo
Muktasari:
- Msimu mpya wa La Liga umeanza wiki chache tu zilizopita, lakini makocha hao tayari wameanza mchakato wa kuanzisha mgomo. Na hiyo inatokana na klabu kadhaa za Ligi Kuu Hispania kushindwa kulipa fidia makocha ziliowafuta kazi.
MADRID, HISPANIA: MAKOCHA Carlo Ancelotti wa Real Mdrid na Hansi Flick wa Barcelona wameripotiwa kuwa na mpango wa kuitisha mgomo.
Msimu mpya wa La Liga umeanza wiki chache tu zilizopita, lakini makocha hao tayari wameanza mchakato wa kuanzisha mgomo. Na hiyo inatokana na klabu kadhaa za Ligi Kuu Hispania kushindwa kulipa fidia makocha ziliowafuta kazi.
Klabu za La Liga zinaruhusiwa kuwafuta kazi makocha wao, lakini suala la kulipa fidia ni lazima hadi ifunguliwe kesi na kufikia makualiano ya kiwango gani cha pesa kitalipwa.
Na sasa mgogoro umeibuka baada ya makocha kuhitaji fidia zilipwe mara tu mtu anapofukuzwa kazi. Baadhi ya makocha waliofutwa kazi ni pamoja na Quique Setien na Alvaro Cervera, ambao walionyeshwa milango ya kutokea Barcelona na Oviedo mtawalia.
Makocha waliobaki kwenye ajira hawapendezwi na jambo hilo la watu kucheleweshewa malipo yao ya fidia na hivyo wamepanga kulizungumza hilo kwenye mkutano wao wa mwaka utakaofanyika wiki hii.
Na katika kutafuta namna ya kumaliza tatizo hilo, makocha mahiri akiwamo Ancelotti na Flick wametishia kuingia kwenye mgomo wakati mkutano na mabosi wa LaLiga utakapofanyika. Zaidi ya makocha 40 wameripotiwa kuwa tayari kuingia kwenye mgomo huo, akiwamo Diego Simeone wa Atletico Madrid.