Amorim: Mastaa wangu wameniudhi!
Muktasari:
- Sougountou Magassa alifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 83 na kuigomea Man United kupata ushindi ambao ungeifanya kupanda hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na kuweka hai matumaini yao ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA, Ruben Amorim amekiri kuhuzunishwa na kukasirishwa baada ya Manchester United kutoka sare ya bao 1-1 na West Ham United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Old Trafford, usiku wa Alhamisi.
Sougountou Magassa alifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 83 na kuigomea Man United kupata ushindi ambao ungeifanya kupanda hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na kuweka hai matumaini yao ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Matokeo hayo ni mara ya nne tangu mwezi uliopita Man United imepoteza fursa ya kupanda hadi kwenye nafasi ya tano ya msimamo wa ligi.
Mashabiki wa Man United waliwazomea wachezaji wa timu hiyo baada ya filimbi ya mwisho huku timu hiyo ikiwa imepata ushindi kwenye mechi moja tu kati ya tano za mwisho. Kocha Amorim amechukizwa na kitendo cha wachezaji wake kushindwa kuwa washindani kwenye kuwania mipira inayozagaa, kitu ambacho anaamini kilichangia kupatikana kwa kona ambayo ilimsaidia Magassa kufunga.
“Nimehuzunika na nimekasirika, ni hivyo,” alisema Amorim.
“Pengine baada ya bao la kwanza, tulipoteza mipira iliyokuwa ikizagaa na Matheus (Cunha) alipata nafasi ya kushinda mpira mmoja au miwili iliyokuwa ikizagaa na kuanzisha mashambulizi. Tulijaribu kujilinda tukiwa mbali ya goli kwa sababu tulifahamu walikuwa wakitaka kupiga krosi na kupata kona.
“Imeshatokea, mipira mirefu, walishinda mipira iliyokuwa ikizaa kona mara tatu dhidi ya wachezaji wetu kwenye eneo la ulinzi, hivyo tulihitaji kuwa vizuri kwenye kipindi cha pili.”
Katika mechi hiyo, Man United ilifanya mabadiliko ya wachezaji watano, wanne ni kwenye eneo la ulinzi. Leny Yoro aliingia kuchukua nafasi ya beki wa kati, Ayden Heaven wakati huo mechi ilikuwa bado hakuna bao lililofungwa, lakini beki wa kushoto Patrick Dorgu na kiungo mkabaji Manuel Ugarte waliingizwa baadaye. Beki wa kati, Lisandro Martinez aliingia baada ya West Ham kusawazisha.
MECHI ZIJAZO ZA MAN UNITED
-Desemba 8 vs Wolves (ugenini)
-Desemba 15 vs Bournemouth (nyumbani)
-Desemba 21 vs Aston Villa (ugenini)
-Desemba 26 vs Newcastle (nyumbani)
-Desemba 30 vs Wolves (nyumbani)