Amorim awasifu mastaa Man United

Muktasari:
- Man United ilicheza na wachezaji 10 kwa dakika 61 baada ya Diogo Dalot kupewa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi Mikel Merino.
MANCHESTER, ENGLAND: Kocha wa Manchester United Ruben Amorim, amewapongeza wachezaji wake baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Arsenal, akisema walistahili kwa kuwa kila mmoja alionyesha hali ya kuipambania timu.
Manchester United ilifanikiwa kuichapa Arsenal kwa penalti 5-3 baada ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Emirates kumalizika kwa sare ya bao 1-1, matokeo yaliyoipeleka United hatua ya nne ya Kombe la FA.
Man United ilicheza na wachezaji 10 kwa dakika 61 baada ya Diogo Dalot kupewa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi Mikel Merino.
Huu ni mchezo wa pili ndani ya muda mfupi kati ya Arsenal na Man United baada ya awali United kuchapwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England Desemba 4, kikiwa ni kipigo cha kwanza cha kocha Amorim tangu alipojiunga na United.
‘Tulionyesha hali ya kupambana sana tofauti na mechi ya kwanza ambayo tulicheza na Arsenal, pamoja na kwamba tulicheza tukiwa na wachezaji kumi uwanjani, lakini hali yetu ya kujituma ilikuwa ya kiwango cha juu na kila mmoja alionyesha uwezo wake.
"Tumeanza kubadilika kwenye eneo hilo na natakiwa kukiri kuwa tulikuwa na wakati mgumu sana mwanzoni mwa mchezo huu.
"Arsenal walikuwa na wachezaji wengi ambao walitumika sana kuutawala mchezo, lakini tuliweza kuwadhibiti kwa kuwa kila mmoja alionyesha juhudi zake uwanjani, kama tukicheza hivi nafikiri tunaweza kuwa bora zaidi huko mbele," alisema kocha huyo ambaye hivi karibuni timu yake ilitoka sare ya mabao 2-2 na Liverpool.
Kocha huyo ambaye alijiunga na United akitokea Sporting Lisbon, alisema wachezaji wake kuna muda walionekana kuchoka lakini kuanzia mwanzoni alishaona kuwa wanaweza kufanya vizuri kwenye mchezo huo na ndicho kilichotokea.
Kwa upande wa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta ambaye alifanikiwa kutwaa ubingwa huo mwaka 2020, likiwa ndiyo kombe pekee alilotwaa akiwa na timu hiyo, alisema haamini kama timu yake imepoteza mchezo huo kwa kuwa ilionyesha uwezo wa juu.
‘Siamini kama tumepoteza mchezo huu, hakika ukiangalia kiwango tulichoonyesha na matokeo tuliyopata ni vitu viwili tofauti kabisa, nawapenda wachezaji wangu, naipenda timu hii, naamini ni sehemu ya mchezo na hakika hata ukicheza michezo 1000 unaweza kupoteza mmoja na huo mmoja ndiyo huu," alisema Arteta.
Sasa hatua inayofuata Manchester United itavaana na Leicester mwanzoni mwa mwezi ujao,mchezo ukipigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Ratiba ya mechi nyingine kubwa:
Brighton vs Chelsea
Plymouth Argyle vs Liverpool
Everton vs Bournemouth
Aston Villa vs Tottenham
Leyton Orient or Derby vs Manchester City
Doncaster Rovers vs Crystal Palace
Stoke City vs Cardiff City.