Amorim athibitisha Man United kucheza na Al-Nassr
Muktasari:
- Kauli ya kocha huyo wa Kireno imethibitisha uvumi uliokuwa ukienea kwamba Mashetani Wekundu wanaweza kukutana na Al-Nassr anayoichezea Cristiano Ronaldo, baadaye msimu huu.
KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amethibitisha kuwa kikosi hicho kinapanga kuandaa mechi za kirafiki katikati ya msimu ili kuongeza mapato, kutokana na ukosefu wa ushiriki kwenye mashindano ya Ulaya.
Kauli ya kocha huyo wa Kireno imethibitisha uvumi uliokuwa ukienea kwamba Mashetani Wekundu wanaweza kukutana na Al-Nassr anayoichezea Cristiano Ronaldo, baadaye msimu huu.
Manchester United haishiriki michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 11, baada ya kumaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Tumaini la Man Unitd kufuzu michuano ya Ulaya lilikuwa kupitia Europa League, lakini ilipoteza fainali dhidi ya Tottenham Hotspur.
Kutokana na kushindwa kufuzu kwa mashindano yoyote ya Ulaya, United itakuwa na wiki nyingi za mapumziko katikati ya msimu. Kwa sababu hiyo, taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo inachunguza uwezekano wa kucheza mechi ya kirafiki nchini Saudi Arabia.
Mazungumzo na wadau husika yanaripotiwa kuwa yanaendelea, na safari ya kwenda Mashariki ya Kati huenda ikawa fursa ya Manchester United kukutana tena na Cristiano Ronaldo, ambaye aliachana na klabu hiyo kwa hali ya sintofahamu mwaka 2022.
Katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Sunderland itakayochezwa leo, Ruben Amorim aliulizwa kuhusu taarifa hizo.
Amorim amesema: "Lazima tufanye hivyo. Tulijua tangu tulipokosa nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya, na kuna mambo mengi ya kuzingatia. Tuna mashabiki wetu huko, tunapaswa kufidia mambo mengi. Tunapaswa kufanya hivyo, kwa hiyo tutafanya. Tunataka kuwa na mashabiki wetu duniani kote, kwa hiyo tutapanga yote ili yatekelezeke. Tukilazimika kufanya hivyo, ni juu yetu kupanga ratiba vizuri."
Uwezekano wa Ronaldo kukabiliana na klabu hiyo aliyowahi kuitumikia ni jambo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki pamoja na vituo vya matangazo karibu duniani kote.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40, alichezea Manchester United katika vipindi viwili tofauti, awali ilikuwa mwaka 2003 hadi 2009 alipotimkia Real Madrid, baadaye akatua Juventus, kisha akarejea Old Trafford mwaka 2021 na kuondoka 2022 alipojiunga na Al Nassr alipo sasa.