Amorim anajua hili? Historia ya makocha Man United na vipigo vya Liverpool
Muktasari:
- Kwa kipindi hicho, Man United ilikuwa juu ya Liverpool kwenye msimamo wa ligi na ligi ilipomalizika, miamba hiyo ya Old Trafford iliachwa nyuma kwa pointi nane.
LIVERPOOL, ENGLAND: RUBEN Amorim anajua hii? Kama hajui iko hivi, chama lake la Manchester United linakwenda Anfield kuwakabili Liverpool, ambao ni maspeshalisti wa kufukuzisha makocha wa Old Trafford.
-David Moyes alifutwa kazi siku 37 baada ya kipigo cha 3-0.
-Louis van Gaal alipigwa kibuti siku 68 baada ya kichapo cha 2-0
-Jose Mourinho alifukuzwa siku mbili baada ya kuchapwa 3-1.
-Ole Gunnar Solskjaer alifukuzwa siku 28 baada ya kipigo cha 5-0.
-Ralf Rangnick aliondolewa siku 40 baada ya kipigo cha 4-0
-Erik ten Hag alifukuzwa siku 57 baada ya kipigo cha 3-0
Katika siku ambayo Man United ilichapwa 3-0 na Liverpool ikiwa chini ya Erik Ten Hag, mkurugenzi mtendaji mkuu, Omar Berrada, aliwaambia waandishi bodi ya timu inamsapoti kocha huyo kabla ya mechi haijaanza. Lakini, wiki nane baadaye, Ten Hag akaonyeshwa mlango wa kutokea.
Kushuka kiwango cha Man United chini ya kocha huyo Mdachi kulianzia Anfield kwenye kipigo cha mabao 7-0, Machi 2023.
Hiyo ilikuwa wiki moja baada ya Ten Hag kuisaidia timu hiyo kumaliza ukame wa miaka sita wa kutobeba taji, wakati iliponyakua Kombe la Ligi.
Kwa kipindi hicho, Man United ilikuwa juu ya Liverpool kwenye msimamo wa ligi na ligi ilipomalizika, miamba hiyo ya Old Trafford iliachwa nyuma kwa pointi nane. Baada ya kipigo kile cha Anfield, Man United ilikwenda kushinda mechi 11 kati ya 22 na ilimaliza vibaya zaidi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 34, ilipomaliza msimu wa 2023-24 kwenye nafasi ya nane.
Liverpool inaonekana kama vile imekuwa ikishikilia mikataba ya makocha wa Man United na sasa zamu ya Amorim kujinasua kwenda Anfield, mahali ambako mara ya mwisho Mashetani Wekundu kushinda hapo ilikuwa Januari 2016.
Man United imecheza mechi 10 bila ya kushinda uwanjani hapo, ikiwani ni kipindi kirefu zaidi kwa timu kushindwa kupata ushindi kwenye uwanja mmoja katika historia yao.
Balaa ni Liverpool itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi mbili mfululizo kwenye ligi, Crystal Palace na Chelsea, huku ikiwa ilipoteza pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray, hivyo kumfanya kocha Arne Slot kupoteza mechi tatu zilizopita.
Liverpool imekuwa gundu kwa Man United kwa miaka ya karibuni. Mechi ambazo Man United ilichapwa na Liverpool ilimalizika kwa matokeo ya makocha kufutwa kazi huko Old Trafford na zile mbili ambazo Man United ilienda Anfield na kugoma kupoteza, ilimaliza nafasi ya nane na 15.
Ilitoka sare ya 0-0, Desemba 2023 kabla ya kuibana Liverpool na kufungana 2-2, Januari mwaka huu. Je, safari hii itakuwaje wakati miamba hiyo itakapokutana huko Anfield, Jumapili?