Amorim amvulia kofia Fernandes

Muktasari:
- Man United ilishuhudia ikicheza mechi ya saba bila ya kupoteza kwenye michuano yote katika mechi hiyo iliyofanyika King Power, ambapo Fernandes aliasisti mara mbili na kufunga mara moja akiisaidia timu hiyo ya Amorim kupanda hadi nafasi ya 13.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amemsifu Bruno Fernandes na kusema ni mtu spesho kabisa baada ya nahodha huyo wa Mashetani Wekundu kuiongoza miamba hiyo kupata ushindi mnono wa wa 3-0 dhidi ya Leicester City kwenye Ligi Kuu England, Jumapili.
Man United ilishuhudia ikicheza mechi ya saba bila ya kupoteza kwenye michuano yote katika mechi hiyo iliyofanyika King Power, ambapo Fernandes aliasisti mara mbili na kufunga mara moja akiisaidia timu hiyo ya Amorim kupanda hadi nafasi ya 13.
Ramus Hojlund na Alejandro Garnacho walimaliza ukame wa mechi 21 na 25 za bila ya kufunga mtawalia, lakini kocha Amorim amemwaga sifa nyingi kwa nahodha wake wa kikosi.

"Bruno ni mtu spesho," alisema Amorim na kuongeza. "Siku zote yupo tayari. Siku zote namwona Bruno ambaye ni hatari anaposhambulia na Bruno ambaye ana uwezo wa kukaba katika hali zote. Kitu ambacho ananishangaza ni jinsi anavyofanya kazi, ananishangaza sana."
Fernandes, ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi, alisema: "Nadhani unaweza kuona jinsi tunavyosonga mbale, lakini hii kitu lazima iendelee. Tuna mechi muhimu sana. Nataka kufunga mabao mengi kwa kadri ninavyoweza. Hilo ni jambo muhimu kwa upande wangu na nataka kuasisti kwa wengine pia. Nataka kusogelea kwenye boksi la wapinzani na kufunga mabao, huo ndio ubora wangu."

Huzuni pekee kwenye mechi hiyo ya Man United ni kumpoteza beki wao kinda, Ayden Heaven, 18, ambaye alitoka uwanjani akiwa amebebwa kwa machela kutokana na kuumia.