Amorim amtaja mchawi Man United

Muktasari:
- Man United ilikumbana na kipigo hicho uwanjani City Ground, shukrani kwa bao pekee la staa wa zamani wa Old Trafford, Anthony Elanga, aliyeifungia Forest kwa jitihada binafsi katika dakika ya tano na kukiacha kikosi cha kocha Amorim kikibaki kwenye nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu England, ambako inaweza kushuka zaidi baada ya mechi za Jumatano usiku.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim ametaja kinachoigharimu timu yake msimu huu huku akiwachana wachezaji wake baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Nottingham Forest katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika City Groud, Jumanne usiku.
Man United ilikumbana na kipigo hicho uwanjani City Ground, shukrani kwa bao pekee la staa wa zamani wa Old Trafford, Anthony Elanga, aliyeifungia Forest kwa jitihada binafsi katika dakika ya tano na kukiacha kikosi cha kocha Amorim kikibaki kwenye nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu England, ambako inaweza kushuka zaidi baada ya mechi za Jumatano usiku.
Matokeo hayo yana maana kwamba Amorim ameshinda mechi sita tu kati ya 19 alizoiongoza Man United kwenye Ligi Kuu England na inakoelekea itakwenda kumaliza ligi kwenye 10 la chini kwa mara ya kwanza tangu 1989-90.
Kocha, Amorim amewaanyoshea vidole wachezaji wake kutokana na kiwango walichoonyesha kwenye mechi hiyo ya kipigo, akidai kwamba waliisaidia Forest kupata pointi tatu.
“Tulitawala mchezo, lakini tayari tulikuwa tunaifahamu hii Forest inaweza kufunga bao kwenye mazingira yasiyoeleweka,” alisema Amorim na kuendelea. “Walipofunga bao, tulibadili mchezo kutoka vile walivyokuwa wakitaka.
“Tulijaribu kutengeneza nafasi, lakini tulipofika kwenye eneo lao, pasi zetu za mwisho, hatukuwa na asisti. Unaposhindwa kuwa na asisti huwezi kufunga mabao. Msimu huu, mambo yamekuwa hivyo. Tumepiga mashuti mengi sana, tumekuwa tukiwabana wapinzani kwenye goli lao, lakini kwenye lile eneo tumeshindwa.”
“Tunahitaji kushinda mechi na tulistahili la ziada kwenye hii mechi, hilo lipo wazi, lakini kosa letu, tunahitaji kuwa makini tunapokaribia goli la wapinzani. Tungeshinda hii mechi, sio kutoa sare, lakini mwisho wa mechi, tumepoteza pointi zote tatu.
“Tunafahamu tabia za timu, bao moja wao linawaweka kwenye mazingira wanayotaka. Yatupasa kufunga mabao mawili kushinda mechi na hapo ndipo tatizo linapoanzia. Tuliwasaidia kupata pointi tatu.”
Alipoulizwa kuhusu rekodi zake Man United, kocha Amorim alisema timu yake anaona inapiga hatua vizuri na kuzipuuza taarifa za kukosolewa, akisema: “Nimeona kitu kwenye hii mechi. Siwezi kujidanganya mwenyewe, watu waache waseme wanachotaka, lakini tunachohitaji sisi ni kushinda mechi. Tuna mechi nyingine mbele yetu, akili yetu imeelekezwa huko.”
Man United itakipiga na Manchester City kwenye Manchester derby Jumapili kabla ya kukipiga kwenye mchakamchaka wa Europa League dhidi ya Lyon ugenini, Alhamisi ijayo. Man United inahitaji ubingwa wa Europa League ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.