Amorim afunguka kuuza mastaa United
Muktasari:
- Bosi huyo wa Old Trafford anafahamu wazi kikosi chake kinahitaji straika mpya na usajili wa mastaa wengine kibao ili kuja kuijenga timu kuwa bora kutoka kwenye hali ya sasa.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA, Ruben Amorim amekiri kwamba ataendelea kuuza mastaa wake ili apate pesa ya kusajili wengine huku hilo likituma ujumbe wa wazi namna Manchester United ilivyotikisika kiuchumi.
Bosi huyo wa Old Trafford anafahamu wazi kikosi chake kinahitaji straika mpya na usajili wa mastaa wengine kibao ili kuja kuijenga timu kuwa bora kutoka kwenye hali ya sasa.
Lakini, kusajili nyota wapya ni wazi atalazimika kushuhudia baadhi ya mastaa wake matata wakiachana na timu hiyo kwenye dirisha la majira ya kiangazi ili kupata pesa.
Kocha Amorim alisema: “Lazima nikubaliane na matatizo haya ambayo klabu inakabiliana nayo na uzuri ni kwamba si jambo jipya. Kama unavyofahamu sheria ya matumizi, tuna tatizo kwa sasa, hivyo tujipe presha sana, tuangalie mambo mengine kama mechi ya Tottenham, Jumapili.
“Kitu rahisi ni kwamba, ili kusajili ni lazima uuze wachezaji. Kwa sasa dirisha limefungwa.”
Man United ipo kwenye mchakato wa kupunguza matumizi, jambo linalomfanya mmiliki wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe kufikiria kuwafuta kazi wafanyakazi wengine 200 tofauti na wale 250.
Mshahara wa Pauni 2 milioni kwa mwaka aliyokuwa akilipwa Sir Alex Ferguson kama balozi wa klabu hiyo nao umefutwa. Man United imepoteza Pauni 300 milioni kwenye kipindi cha miaka mitatu, jambo linalowaweka kwenye wasiwasi wa kukumbana na adhabu ya kupokwa pointi.
Katika kuifanya klabu kuepuka adhabu kama hiyo ndipo uamuzi wa kupunguza wafanyakazi unapokuja, sambamba na kuuza wachezaji ili kufanya vitabu vyao vya kifedha kuwa vizuri.
Kwenye mchakato wa kuuza wachezaji, Man United ipo tayari kuwafungulia mlango wa kutokea makinda wake Kobbie Mainoo na Alejandro Garnacho kama kutakuwa na pesa nzuri mezani, ambapo ripoti zinafichua yenyewe inataka Pauni 65 milioni kwa kila mchezaji.
Kwenye dirisha la Januari, Man United imepunguza kiasi bili yao ya mishahara baada ya kuwatoa kwa mkopo Marcus Rashford na Antony waliokwenda Aston Villa na Real Betis mtawalia – huku jambo hilo likiwawasidia kupunguza Pauni 300,000 kwa wiki kwenye bili ya mishahara.