Aliyegoma kunyoa nywele hadi United ishinde tano
Muktasari:
- Ikiwa Man United itapata ushindi mbele ya West Ham, Frank atakata nywele zake na kuzitoa kama msaada kwenda Little Princess Trust, shirika lisilo la kiserikali la Uingereza.
MANCHESTER, ENGLAND: SHABIKi wa Manchester United , Frank Ilett, ambaye amegoma kunyoa hadi timu hiyo ishinde mechi tano mfululizo amefunguka na kusema sasa anaona kabisa jambo lake linakwenda kutimia.
Ilett hajanyoa nywele kwa takribani siku 500, tangu alipotangaza kwamba atanyoa endapo tu Man United itashinda mechi tano mfululizo.
Akizungumzia kiwango cha timu hiyo ambayo imeshinda mechi nne mfululizo chini ya Carrick, shabiki huyo amesema: “Carrick yuko kwenye uelekeo mzuri, nywele hizi nitazinyoa hivi karibuni, West Ham inafuata nina uhakika tutashinda, tayari tumeshashinda nne kati ya tano. Hii ni mara ya kwanza kuwa na ushindi wa mechi nne mfululizo tangu nilipotoa ahadi. Nina uhakika wakati huu inaenda kutokea. Asante sana Carrick asante, asante, asante. Nitaalika mashabiki wenzangu kutazama nao mechi dhidi ya West Ham. “
Frank amekuwa maarufu mtandaoni kadri nywele zake zilivyoendelea kukua, na vyanzo vya ndani vinadai wachezaji wamekuwa wakitamani sana kushinda mechi tano mfululizo ili kumfanya shabiki huyo anyoe nywele.
Chanzo kimoja kiliambia The Sun: “Wachezaji wanafurahia sana mabadiliko ya kikosi na matokeo wanayoyapata. Wanamfahamu vizuri Frank kwa sababu wamemuona huko mitandaoni. Baadhi yao walikuwa wakicheka na kusema, ‘Twende, tumkanyoe nywele huyu shabiki.’”
Frank alianza safari yake Oktoba 05, 2024, wakati Erik ten Hag bado akiwa kocha mkuu ambapo amesema, angekata nywele zake mara tu Man United ingeshinda michezo mitano mfululizo.
Shabiki huyo mzaliwa wa Oxford ambaye kwa sasa anaishi Hispania, hakuwahi tena kunyoa nywele tangu kipindi hicho hata baada ya Erik ten Hag kufukuzwa na Ruben Amorim kuajiriwa.
Chini ya Amorim kuna wakati ilionekana kama ahadi ingeenda kutumia pale timu iliposhinda mechi tatu mfululizo lakini mambo hayakwenda kama yalivyotarajiwa.
Ikiwa Man United itapata ushindi mbele ya West Ham, Frank atakata nywele zake na kuzitoa kama msaada kwenda Little Princess Trust, shirika lisilo la kiserikali la Uingereza.
Shirika hilo linatoa msaada wa nywele bandia kwa watoto waliopoteza nywele zao kutokana na magonjwa.