Aliyechomwa kisu kucheza LIGI YA UEFA

Muktasari:

  • Young alikuwa na umri wa miaka 17 pekee wakati shambulio hilo la kutisha lilipomtokea katika bustani ya  Solihull, Mei 2020.

BIRMINGHAM, ENGLAND: ALIYEKUWA mchezaji wa Aston Villa, Brad Young ambaye aliponea chupu chupu kupoteza maisha baada ya kuchomwa kisu mara tatu sasa anajiandaa kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Young alikuwa na umri wa miaka 17 pekee wakati shambulio hilo la kutisha lilipomtokea katika bustani ya  Solihull, Mei 2020.

Mshambuliaji huyo alifanyiwa upasuaji ili kuokoa maisha yake kwani kisu kiliingia ndani umbali wa sentimita 12 na mbali ya kupasuliwa pia aliongezewa damu mara tatu.

Matumaini ya kwamba ataishi yalipotea kwa muda kutokana na ukubwa wa majeraha lakini alipona na kuendelea kucheza soka.

Sasa, imepita miaka minne na staa huyo anajiandaa kuiongoza safu ya ushambuliaji ya The New Saints  kutoka Wales katika mechi za hatua ya kufuzu za Ligi ya Mabingwa.

Akisimulia tukio hilo, Young alisema: “Nilikuwa kwenye bustani pamoja na marafiki zangu, ghafla  kundi la vijana wa kawaida lilinijia, wakanishambulia na kujaribu kuniibia. Nilijitetea, yule mtu aliyenipiga ngumi usoni alikuwa amenikaba roba shingoni na mara nikahisi kitu cha ajabu mgongoni mwangu, baada ya hapo aliachia na nikagundua nimechomwa kisu mara tatu.”

“Niliita gari la wagonjwa lakini kabla halijaja nilianguka chini. Walinipeleka hospitalini na hawakujua nini kitatokea, jeraha moja la kisu liligonga mshipa na kusababisha nipoteze damu nyingi, lilikuwa limeenda umbali wa sentimita 12  na nilihitaji kuongezewa damu mara tatu, kabla ya kukaa sawa.”

“Nilipokuwa Hospitalini  nilikuwa nauliza kama naweza kucheza tena soka, unajua wakati huo nilikuwa mtu wa starehe sana na nilipenda fujo jambo ambalo sio zuri kwa mchezaji wa umri kama wangu, baada ya hapo nilijifunza na kuwa mtulivu.”