Alexander-Arnold kubadili upepo Liverpool

Muktasari:
- Trent mwenye umri wa miaka 26, hivi karibuni alikuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool kilichotangaza ubingwa baada ya kuichapa Tottenham mabao 5-1 na baada ya mechi inaelezwa wawakilishi wake walikutana na mabosi wa Liverpool kujadili uwezekano wa kumbakisha.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI kisiki wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold ambaye anadaiwa atajiunga na Real Madrid mwisho wa msimu huu, mkataba wake utakapomalizika, huenda mambo yakabadilika na akabaki kwa mujibu wa ripoti.
Trent mwenye umri wa miaka 26, hivi karibuni alikuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool kilichotangaza ubingwa baada ya kuichapa Tottenham mabao 5-1 na baada ya mechi inaelezwa wawakilishi wake walikutana na mabosi wa Liverpool kujadili uwezekano wa kumbakisha.
Inaelezwa Trent anahitaji kulipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko mchezaji yeyote ili kusaini mkataba mpya.
Jambo hilo linaonekana kuwa gumu kwa Liverpool kwani tayari imeshawasaini Virgil van Dijk na Mohamed Salah watakaokuwa wanalipwa Pauni 400,000 kwa wiki kila mmoja.
Trent anaonekana kulainisha moyo wake na kuwa tayari kubakia ikielezwa hali hiyo imechangiwa sana na kiwango cha Real Madrid ambacho imekionyesha msimu huu.
Vilevile staa huyu anasuasua kwa sababu hajui ni kocha gani ataenda kuchukua mikoba ya Carlo Ancelotti anayetajwa kuondoka mwisho wa msimu.
Mchezaji mwenzake Cody Gakpo alionyesha matumaini baada ya mechi, beki huyu anaweza akabakia kwa msimu ujao.
"Nadhani timu haijabadilika sana, kwa hiyo sasa unaweza kujenga juu ya timu hiyo kwa msimu ujao. Sasa Mo na Virgil wamebaki na tunatumai Trent pia atabaki."
Licha ya kutokuzungumza na waandishi wa habari Jumapili, Alexander-Arnold alionekana akizungumza kwa kina na mmiliki wa Liverpool, John W. Henry, jambo lililozua maswali zaidi na matumaini kwa mashabiki wa Liverpool.