Afcon 2025 mambo matamu yanukia
Muktasari:
- Taarifa kutoka Morocco ni kwamba unaposhuka kutoka kwenye ndege, jiji Casablanca kuanzia usiku wa Jumatatu, inakuwa rahisi kwa wageni kujua taifa hilo lipo bize na fainali hizo kwa namna pilikapilika zilivyo.
SAA chache kabla ya kuanza kwa fainali za 35 za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) huko Morocco mambo yameanza kunukia wenyeji wakianzia kwenye viwanja vya ndege.
Taarifa kutoka Morocco ni kwamba unaposhuka kutoka kwenye ndege, jiji Casablanca kuanzia usiku wa Jumatatu, inakuwa rahisi kwa wageni kujua taifa hilo lipo bize na fainali hizo kwa namna pilikapilika zilivyo.
Kabla hata ya mikanda inayozunguka kupitisha mizigo, kabla ya kaunta za uhamiaji, kabla ya kelele za kawaida za kumbi za mapokezi, soka linajitangaza lenyewe.
Mipira mikubwa ya soka yenye nembo ya AFCON imetawala eneo la uwanja wa ndege. Skrini za LED zinamulika rangi za mashindano. Kauli mbiu za kuikaribisha Afrika zinang’aa kwenye kuta na njia za watembea kwa miguu. Kuanzia dakika ya kwanza mashabiki wanapowasili, viwanja vya ndege vya Morocco si vituo vya kupita tena, bali ni sehemu ya mashindano yenyewe.
Fainali za Afcon zitaanza rasmi Jumapili, jijini Rabat kwa mechi ya Kundi A kati ya wenyeji Morocco na Comoros itakayoashiria mwanzo wa mashindano ya wiki nne za kuwania ubingwa.
Mechi hiyo itaanza saa 2:00 usiku kwa saa za Morocco (sawa na saa 4:00 usiku kwa Tanzania) na utashuhudiwa na mashabiki waliojaa katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, huku Morocco ikikaribisha toleo la 35 la mashindano hayo, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka 37.
Kwa kuwa maelfu kwa maelfu ya mashabiki wanatarajiwa kupita katika viwanja vya ndege vya Casablanca, Marrakech, Rabat, Tangier, Fes na Agadir katika siku zijazo, mtandao wa viwanja vya ndege wa Morocco umeingia katika hali kamili ya uendeshaji na sherehe kwa ajili ya mashindano makubwa zaidi barani Afrika.
Mabadiliko haya ni sehemu ya kampeni ya kitaifa iliyoanzishwa na Ofisi ya Kitaifa ya Viwanja vya Ndege (ONDA) chini ya kaulimbiu “Karibu Soka, Karibu Mashabiki”.
Katika taarifa yao, ONDA ilithibitisha kuwa viwanja vya ndege vya Morocco, “viko tayari kikamilifu kutimiza wajibu wao kama lango kuu la kusherehekea Kombe la Mataifa ya Afrika 2025,” kwa kushirikiana kwa karibu na Kamati ya Maandalizi ya Ndani pamoja na CAF.
Katika kumbi za kuwasili, matangazo ya LED yenye mandhari ya AFCON yamewekwa, picha za kuvutia zinawaongoza mashabiki ndani ya vituo, huku miundo mikubwa ikiwemo mipira ya soka na alama za mashindano ikionyesha kuwa mwezi ujao ni mali ya soka la Afrika.
“Unahisi kama mashindano yanaanza mara tu unaposhuka kutoka kwenye ndege,” alisema Joseph Kabongo, shabiki kutoka DR Congo aliyewasili kutoka Kinshasa.
“Hata kabla hujapigwa muhuri wa pasipoti, tayari unahisi hamasa. Ni tofauti na mashindano mengine.”
Nyuma ya pazia, mandhari hii ya sherehe inaungwa mkono na miezi ya mipango ya kiutendaji na maboresho ya miundombinu.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Morocco imepanua uwezo wa viwanja vya ndege, kuboresha mtiririko wa abiria, kuimarisha taratibu za kiusalama na kuongeza idadi ya watumishi waliopata mafunzo maalumu ili kukabiliana na ongezeko la wasafiri.
Mamlaka zinasema juhudi hizi zimehusisha taasisi mbalimbali, zikiwamo Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi la Taifa (DGSN), Gendarmerie ya Kifalme, Forodha pamoja na Wizara ya Uchukuzi na Usafirishaji.
Maeneo maalumu ya mapokezi, mabango ya lugha mbalimbali, timu za msaada zilizoimarishwa na mifumo ya ufuatiliaji wa wakati halisi sasa imewekwa, hasa katika miji inayocheza michezo ya Afcon.