Acha kipigwe! UEFA Champions League kwa moto
Muktasari:
- Usiku wa Jumanne, mashabiki wa soka watashuhudia mechi nne za kibabe sana, huku machi ya wengi yatakuwa huko Uturuki na Galatasaray itajimwaga uwanjani kwao kukipiga na Liverpool katika moja ya mechi za kibabe sana.
LONDON, ENGLAND: ILE siku ulokuwa unangoja, imefika. Ni mtafutano, wakati chama lako unalolifagilia litakapotupa kete yake muhimu katika mechi ya mtoano ya hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, itakapopigwa usiku wa Jumanne na Jumatano. Kazi ipo.
Usiku wa Jumanne, mashabiki wa soka watashuhudia mechi nne za kibabe sana, huku machi ya wengi yatakuwa huko Uturuki na Galatasaray itajimwaga uwanjani kwao kukipiga na Liverpool katika moja ya mechi za kibabe sana.
Mechi hiyo ni ya mapema zaidi ukilinganisha na nyingine zitakazopigwa usiku huo wa Jumanne na huko Italia, shughuli itakuwa pevu uwanjani Gewiss wakati Atalanta itakuwa mwenyeji kuwakabili mabingwa wa kutandaza soka Ujerumani, Bayern Munich.
Ukiachana na balaa hilo, kasheshe jingine litakuwa huko Civitas Metropolitano, wakati jeshi la Diego Simeone lenye staa wa moto kwelikweli kwa sasa, Ademola Lookman litakaposhuka uwanjani kuikabili Tottenham Hotspur inayocheza kwa kiwango cha hovyo sana huko kwenye Ligi Kuu England kwa sasa.
Timu zote zitahitaji ushindi katika mchezo wao wa kwanza wa hatua hiyo ya 16 bora, lakini Spurs itahitaji maoni zaidi kwenye mechi yake hiyo ya ugenini kutokana na kiwango chao cha sasa.
St James’ Park patashuhudiwa kipute kingine matata kabisa na Newcastle United inayotoka kupokea kichapo cha mabao 3-1 katika mechi iliyopita, iliyofanyika uwanjani hapohapo mbele ya Manchester City katika Kombe la FA, sasa itakuwa na kazi pevu zaidi ya kuikabili Barcelona ya Lamine Yamal, ambayo imekuwa na malengo makubwa ya kunasa mataji mawili makubwa inayoyakimbizia msimu huu.
Barca imeshatupwa nje kwenye Copa del Rey, hivyo nguvu ya kunyakua mataji kwa msimu huu sasa imeelekezwa kwenye La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya na usiku wa Jumanne wataanzia kusaka ushindi wao ugenini mbele ya Newcastle. Hilo ni bonge la mechi.
Mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa hatua hiyo ya mtoano itaendelea kwa Jumatano na macho na masikio ya wengi yataelekezwa huko Estadio Santiago Bernabeu, wakati Kylian Mbappe na Vinicius Jr watakapoliongoza chama lao la Real Madrid kukabiliana na Manchester City yenye huduma matata kabisa kutoka kwa straika Erling Haaland.
Mechi hiyo imejaa visa vingi vya kulipa kisasi baada ya msimu uliopita miamba hiyo kukutana kwenye mechi za mtoano na Man City ikatupwa nje ya mashindano.
Wakati mashabiki wakitafakari kile ambacho kinachoweza kwenda kutokea huko Bernabeu, moto mwingine utawashwa huko Parc des Princes, ambapo mabingwa watetezi Paris Saint-Germain watashuka uwanjani kwao kuwakabili Chelsea.
Hiyo ni mechi nyingine ya visasi na miamba hiyo ilikutana kwenye fainali ya Kombe la Dunia la Fifa kwa timu za klabu na Chelsea iliibuka na ushindi wa kibabe kabisa. Safari hii itakuwaje?
Arsenal ambayo ipo kwenye vita ya kufukuzia mataji manne msimu huu haitakuwa na mzaha wakati itakapokwenda Ujerumani kukipiga na Bayer Leverkusen kwenye moja ya mechi zenye mvuto mkubwa katika hatua hiyo ya mtoano, huku kiboko ya vigogo Bodoe/Glimt itakuwa uwanjani kwao kukipiga na wababa wa Ureno, Sporting Lisbon. Mambo ni moto.