AC Milan haitanii kwa Rashford
Muktasari:
- Manchester United inahaha sasa hivi kutafuta timu ya kumchukua Rashford kabla ya dirisha hili la uhamisho wa Januari halijafungwa baada ya fowadi huyo kuwekwa benchi na kocha Ruben Amorim.
MILAN, ITALIA: MAMBO ni moto. AC Milan inajiandaa kuondoa mshambuliaji mmoja kwenye kikosi chake ili kufungua njia ya kumnasa Marcus Rashford.
Manchester United inahaha sasa hivi kutafuta timu ya kumchukua Rashford kabla ya dirisha hili la uhamisho wa Januari halijafungwa baada ya fowadi huyo kuwekwa benchi na kocha Ruben Amorim.
Fowadi huyo Mwingereza, Rashford mwenyewe alishakiri kwamba yupo tayari kwenda kukabiliana na changamoto mpya kwingineko, hivyo akijiweka sawa kwa ajili ya kubadili timu kwenye dirisha hili la Januari na kuachana na maisha ya Old Trafford.
Milan imeonekana ndiyo timu inayohitaji zaidi huduma ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ambaye hivi karibuni aligomea mpango wa kuhamia huko Saudi Arabia na Uturuki akiamini bado hajafikia viwango vya kwenda kucheza kwenye ligi za huko.
Hata hivyo, kinachoweka ugumu wa dili lake kutokea kwenye dirisha hili la Januari ni mshahara wa mchezaji huyo, ambapo analipwa Pauni 325,000 kwa wiki na mkataba wake kwenye kikosi cha Man United utafika tamati Juni 2028.
Miamba hiyo ya Italia inamtaka Rashford kwa mkopo hadi mwisho wa msimu, lakini haipo tayari hata kulipa nusu ya mshahara wa mchezaji huyo, ambapo kwenye kikosi chao mchezaji anayelipwa zaidi ya wengine ni straika, Alvaro Morata, Pauni 150,000 kwa wiki.
Hata hivyo, Milan haijakata tamaa kwenye kufanya mazungumzo na mabosi wa Man United wakiamini kwamba wanaweza kufanikisha kwenye mpango wao huo wa kumchukua Rashford kabla ya dirisha la Januari kufungwa.
Ripoti kutoka Italia zinafichua kwamba fowadi wa Milan, Noah Okafor, jana Ijumaa alitarajia kusafiri kweda Ujerumani kwenda kujiunga kwa mkopo kwenye klabu ya RB Leipzig kwa makubaliano ya kubebwa jumla mwisho wa msimu kwa ada ya Pauni 21 milioni. Fowadi huyo wa Uswisi alijiunga na Milan akitokea RB Salzburg kwa uhamisho wa Pauni 13 milioni mwaka 2023, lakini ameonekana bado hana maajabu makubwa.
Kuondoka kwake kutafanya timu hiyo kuwa na nafasi na hivyo Rashford anaweza kuingia kutokana na ripoti kudai wakala wake, Dane amekwenda Italia kufanya mpango huo. Man United inahitaji kuachana na mchezaji huyo hasa katika kipindi hiki ambacho bilionea mmiliki wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe anajaribu kubana matumizi kwenye kikosi.
Rashford hajaichezea Man United tangu kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Viktoria Plzen kwenye Europa League, Desemba 12. Amechangia mabao 10, akiwa amefunga saba na kuasisti mara tatu katika mechi 24 alizocheza msimu huu na sasa anaelekea mlango uliandikwa ‘exit’ kuachana na klabu hiyo ya utoto wake kabla ya dirisha hili la majira ya baridi halijafungwa Februari 3.
“Kwangu mimi, binafsi, nadhani nipo tayari kwa ajili ya changamoto mpya na kupiga hatua nyingine,” alisema Rashford mwezi uliopita.
“Nitakapoondoka sitakuwa na chuki, sitakwenda kuzungumzia mambo yoyote mabaya kuhusu Manchester United. Ninachokijua mahali hapa mambo yameshakuwa mabaya ni heri niondoke kabla hayajatibuka zaidi. Nimeona wachezaji wakiondoka hapa na kuwa watulivu, hivyo mimi siwezi kuwa tofauti.”