‘Ubaya ubwela’… Njia ya kwenda fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
Muktasari:
- Arsenal, Liverpool, Tottenham, Chelsea na Manchester City zilihakikisha nafasi zao katika hatua ya 16 bora kwa kumaliza ndani ya nane bora kwenye hatua ya makundi.
LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Hii inaitwa ubaya ubwela. Njia ya kila timu ya England kwenda fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu sasa imefahamika.
Arsenal, Liverpool, Tottenham, Chelsea na Manchester City zilihakikisha nafasi zao katika hatua ya 16 bora kwa kumaliza ndani ya nane bora kwenye hatua ya makundi.
Newcastle pia bado ina nafasi ya kufika nchi ya ahadi baada ya kufuzu hatua ya mchujo, pamoja na majina makubwa ya Ulaya.
Sasa, njia ya kila timu kwenda fainali imewekwa wazi kulingana na upangaji wa hatua inayofuata kwa kuzingatia timu zilizofuzu.
1.Njia ya Arsenal; Arsenal ilimaliza kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Kairat, uliowahakikishia rekodi ya asilimia 100.
Baada ya kuruka hatua ya mchujo, Arsenal sasa inasubiri hatua ya 16 bora na wanaweza kukutana na ama Atalanta, Bayer Leverkusen, Borussia Dortmund au Olympiacos.
Kwenye Robo fainali inaweza kuileta Arsenal dhidi ya Man City, iwapo Man City itafanikiwa kuishinda Real Madrid, Inter Milan au Sporting Lisbon.
Kisha, nusu fainali inaweza kuleta pambano dhidi ya Chelsea au Tottenham, huku Liverpool na Barcelona pia wakiwa kwenye mbio, pamoja na PSG na Newcastle.
Hatimaye, Arsenal inaweza kuandaliwa pambano la fainali dhidi ya adui wa zamani, Harry Kane na chama lake la Bayern Munich.
2.Njia ya Chelsea; Kwa Chelsea, hatua ya 16 bora inaweza kuwaleta dhidi ya PSG, Newcastle, Monaco au Qarabag. Liverpool au Spurs huenda wakakutana katika robo fainali, huku Arsenal na Man City wakivizia kwenye nusu fainali.
Bayern Munich, Sporting Lisbon, Real Madrid na Inter Milan pia ni wagombea wa kufika nne bora. Chelsea wanaweza kukutana na yeyote kati ya hao kwenye fainali, pamoja na Barcelona, ambao wanaweza kukutana nao tu katika mchezo wa mwisho.
3.Njia ya Man City; Kwa Manchester City, inaweza kucheza dhidi ya Real Madrid, Inter Milan, Bodoe/Glimt au Benfica katika hatua ya 16 bora.
Arsenal au Bayern Munich zinaweza kuwangoja kwenye robo fainali, huku nusu fainali zikiwaleta Liverpool, Spurs au Chelsea.
Kama Chelsea, Man City pia inaweza kukutana na yeyote kati ya hao kwenye fainali, pamoja na Sporting Lisbon, ambao wanaweza kukutana nao tu kwenye fainali pia.
4.Liverpool na Tottenham (Ratiba sawa); Kwa kushangaza, Liverpool na Tottenham zina droo inayofanana kabisa baada ya kumaliza nafasi ya tatu na ya nne kwenye msimamo wa hatua ya ligi.
Hii ina maana timu hizo haziwezi kukutana hadi fainali huko Budapest.
Kabla ya hapo, kila upande unaweza kukutana na Juventus, Atletico Madrid, Club Brugge au Galatasaray katika hatua ya 16 bora. Robo fainali zinaweza kuwaleta dhidi ya Chelsea, Barcelona, PSG au Newcastle.
Na katika nusu fainali zinaweza kuwaleta Arsenal, Bayern Munich, Man City au Sporting Lisbon, pamoja na Real Madrid na Inter Milan. Kama ilivyo kwa timu nyingine za England, wote hawa ni wapinzani wanaowezekana kwa Liverpool na Spurs kwenye fainali.
5.Njia ya Newcastle; Hatimaye, Newcastle inakabiliwa na safari ndefu zaidi kwenda Hungary kwani lazima waanze na hatua ya mchujo.
Toon watakutana na Monaco au Qarabag, na mshindi atakutana na Chelsea au Barcelona katika hatua ya 16 bora.
Hii ina maana pambano la Waingereza watupu dhidi ya Spurs au Liverpool linaweza kuwangoja kwenye robo fainali. Nusu fainali zinaweza kuwaleta dhidi ya Arsenal, Bayern Munich, Man City au Sporting Lisbon, huku Real Madrid na Inter Milan pia wakiwa chaguo. Kwa mara nyingine, Newcastle inaweza kukutana na yeyote kati ya hao kwenye fainali, pamoja na PSG, ambao inaweza kukutana nao tu kwenye mchezo wa mwisho wa mashindano.