‘Pambano la utani’ Anton Joshua, Jake Paul
Muktasari:
- Licha ya ukosoaji, wapo wengine wanaoamini kwamba pambano hilo ni sehemu ya burudani na biashara, na Joshua anachukua nafasi ya kutengeneza fedha na rekodi zaidi kabla ya mapambano makubwa yajayo.
MIAMI, MAREKANI: ANTHONY Joshua anarejea ulingoni baada ya mapumziko ya miezi 15 kuzichapa na Jake Paul katika pambano litakalofanyika Desemba 19, mwaka huu mjini Miami, Marekani.
Pambano hilo litakalorushwa moja kwa moja duniani kote kupitia Netflix likiwa moja ya mapambano makubwa zaidi ya burudani na biashara mwaka huu, ni kama mwendelezo wa kile ambacho ulimwengu wa masumbwi kwa sasa unakiita kama utani wa kimichezo kutokana na mabondia husika kulenga zaidi fedha kuliko uhalisia wa upinzani na ushindani ulingoni.
Joshua hajapigana tangu Septemba 2024 alipochezea knockout kwa Daniel Dubois, na sasa anatarajia kurudi, huku Jake aliyepaswa kupigana na Gervonta Davis alishindwa kuzichapa baada ya Davis kukumbwa na tuhuma mahakamani hivyo kumfungulia nafasi pambano na Joshua.
Tofauti ya miili kati ya Jake na Joshua ni kubwa, kwani Joshua ana uzito mkubwa na urefu wa ziada kulinganisha na mpinzani wake sambamba na wapinzani wake wa awali.
Joshua alikwea katika uzani wa kilo 109 pambano la mwisho, jambo linalomfanya awe na faida kubwa ya nguvu dhidi ya Jake.
Ingawa kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba halitakuwa la maonyesho, bali kamili la kulipwa linaongeza utata na mjadala katika ulimwengu wa ngumi na hasa kuhusiana na masuala ya kifedha kutangulizwa zaidi mbele kuliko uhalisia wa mambo ya kiufundi kabla na wakati wa kuzichapa.
Jake amekaririwa akisema anaamini akimshinda Joshua atathibitisha thamani yake na kufungua njia ya kupigania ubingwa wa dunia siku chache zijazo.
Kwa upande wake, Joshua amesema anarejea ulingoni bila huruma na anataka kupiga mtu kwa uhakika na kwamba hataki masihara katika kazi yake iliyomfanya awe maarufu duniani.
Hata hivyo, Joshua alidai kwamba huu ni wakati wake wa kufanya mapambano makubwa ya kibiashara na anaamini ataendelea kuvunja rekodi katika mchezo wa ngumi kwa kupigana na mabondia wa aina tofauti.
Uzoefu wa Jane katika uzito wa juu ni mdogo akiwa amepigana pambano moja dhidi ya Mike Tyson mwenye miaka 59 na hii inaonyesha kuna pengo kubwa la uwezo na uzoefu kati ya wawili hao. Joshua ametwaa taji la dunia mara mbili akizichapa na majina makubwa katika ngumi kama Wladimir Klitschko na Joseph Parker.
Wachambuzi wadai pambano hilo halipaswi kuidhinishwa na mamlaka za masumbwi duniani kwa sababu ya hatari kubwa kwa Jake wakimuona Joshua kuwa bondia mwenye nguvu na uwezo wa kimbinu, hivyo lolote linaweza kutokea dhidi ya mpinzani wake hususani kumudu au kutomudu ama kuishia kupoteza maisha ulingoni.
Licha ya ukosoaji, wapo wengine wanaoamini kwamba pambano hilo ni sehemu ya burudani na biashara, na Joshua anachukua nafasi ya kutengeneza fedha na rekodi zaidi kabla ya mapambano makubwa yajayo.