Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIDUKU: Ngumi kuna rushwa, mikataba ya malikauli -2

Muktasari:

  • “Maisha yetu yanahitaji kujitoa sana ili ufanikiwe. Hivi ninavyokwambia, kuna mabondia wanatoa fedha zao mfukoni ili kushiriki mapambano. Hii yote ni kutafuta kujulikana, hivyo sio rahisi kutoka,” anasema na kuongeza:

JANA katika makala ya mahojiano na bondia Twaha Kassim 'Kiduku' alizungumzia mambo mbalimbali ikiwamo gari alilozawadiwa baada ya kumchapa Dulla Mbabe lilipo, msosi na maisha yake mengine. Leo, mkali huyo mwenye mikanda tisa ndani ya ngumi anaendelea kuzungumia yaliyo nyuma ya mchezo huo hapa nchini... Twende pamoja!


MABONDIA KUTOA HONGO ILI WATOKE

Kutengeneza jina si rahisi kama wengi wanavyoamini kwamba ukiwa na kipaji inatosha kujitangaza mwenyewe na kujulikana. Sio hivyo, kama anavyothibitisha Twaha Kiduku, anayesema kuna mabondia wanadiriki kutoa fedha ili washiriki mapambano.

“Maisha yetu yanahitaji kujitoa sana ili ufanikiwe. Hivi ninavyokwambia, kuna mabondia wanatoa fedha zao mfukoni ili kushiriki mapambano. Hii yote ni kutafuta kujulikana, hivyo sio rahisi kutoka,” anasema na kuongeza:

“Ni mtihani sana kutoka. Mabondia wote wanaoanza kujitafuta hawapati fedha kubwa kama Watanzania wanavyoamini. Bondia hawezi kutoka chini hadi kupata Sh1 milioni. Hakuna promota anaweza kumpata na kufanya naye kazi.”

KIDU 01

MIKATABA MALI, KAULI IPO

Kuna mabondia wamekuwa wakidhulumiwa bila ya huruma, kwa mujibu wa Kiduku ambaye anasema alishawahi kupigana hadi kwa kujitolea bila kulipwa chochote, ukiondoa kudhulumiwa.

“Dhahabu haiwezi kuitwa dhahabu bila kupita kwenye moto. Hadi unaona nyani kazeeka, basi kakwepa mishale mingi. Nimepita kwenye changamoto nyingi sana hadi nimefikia hapa. Muda mwingine tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai,” anasema na kuongeza:

“Nimedhulumiwa sana na kutapeliwa. Kuna pambano nilivunjika mkono, hilo hakuna nilichopata. Kaka yangu ndiye alipambana kuniuguza. Kwahiyo ni hekaheka mpaka mtu anafanikiwa, kapitia mengi.”

Anasema kwenye kazi zao kuna hekaheka nyingi, na mpaka anapofanikiwa, anakuwa kapitia shida nyingi. Muda mwingine anapigana kwa hasira ili tu kuweza kufikia malengo yake.


KUUZA MAPAMBANO

Maneno mengi yamekuwa yakizungumzwa kwa mabondia kutoka Tanzania kushindwa kufanya vizuri wakipata mapambano nje ya nchi, huku mengi yakizungumzwa juu ya kuuza mapambano. Twaha Kiduku amethibitisha hilo kwa kuweka wazi kuwa ngumi ni biashara.

“Hayo mambo yapo, ila kwa upande wangu haijawahi kutokea. Ngumi ni biashara, hivyo kila kitu kinaweza kufanyika, lakini mimi sijawahi kufanya hivyo,” anasema Twaha Kiduku.

KIDU 03

ELFU 20 HADI MAMILIONI

Iliwahi kuibuka mijadala mingi baada ya bondia kufariki na kukamilishiwa kiasi cha fedha akiwa amepoteza maisha. Bondia Twaha Kiduku ameamua kutolea ufafanuzi hilo akisema hata yeye hadi kufikia hapo alipo, alianza kucheza bure.

“Kuna msiba wa bondia uliotokea hivi karibuni akiwa jukwaani mwaka huu. Alikuwa amepewa fedha yake nusu ya pambano na kwenda kumaliziwa kiasi kilichobaki msibani. Kiasi cha pambano kilikuwa ni Sh70,000. Watu walizungumza mengi sana,” anasema na kuongeza:

“Mtu kapoteza maisha kwa ajili ya laki moja. Cha ajabu, kuna mabondia wakubwa ambao wamepata majina kupitia mchezo huo na wao walikuwa wanatoa maneno ya ovyo. Mimi nataka kusema, ngumi ni mchezo wa kimasikini sana, ni mchezo wa mtu ambaye kashindwa kufanya kila kitu.”

Twaha Kiduku anasema watu wengi walioingia huko wametoka kwenye hali mbaya, akimtolea mfano bingwa wa zamani wa dunia wa uzito wa juu, Mike 'Iron' Tyson kuwa alipopata fedha kutokana na ngumi, mwanaye alipotaka kuingia kwenye ngumi alimhoji anataka akafuate nini na kumuonya kuwa akiingia kwenye ngumi ataenda kukutana na watu maskini wenye njaa watamuumiza, na kumsisitiza atumie pesa zake.

“Mimi nakumbuka pambano la kwanza nilipewa elfu 20. Nyuma tayari nilikuwa nimeshacheza mapambano mengi ya bure, ambayo ilifika kipindi nilitaka kukata tamaa. Baba aliniambia nipambane nitafute jina, ndiyo nitapata hela, huku akinisisitiza kuwa siwezi kupata hela bila kutengeneza jina,” anasema na kuongeza:

“Kauli kubwa ya baba yangu, ambayo inaishi hadi sasa, ilikuwa ananisisitiza kwa kuniambia nitafute jina. Siwezi kupata fedha nyingi nikiwa sijulikani; nitaishia kuwaona wenzangu wakipata nyingi.”

Kiduku anasema kauli hiyo ilimuongeza njaa ya kupambana zaidi, kufanya mazoezi na kupata mapambano mengi ambayo yalimpa jina kutokana na kushinda mara kwa mara. Ndipo jina lake lilipokua kwa kasi zaidi. Mungu alimjaalia, amekuwa maarufu na anatambulika.

“Baada ya jina langu kukua na kutambulika zaidi ndani na nje, najipangia kiasi ninachotakiwa kukipata kulingana na mapambano. Sijitambi, lakini nafurahia huu mchezo umenipa maisha na nimechezea pesa nyingi. Kwa Tanzania hakuna bondia anayenifikia.”

Kiduku anasema baada ya kupata Sh20,000 na kupambana zaidi kutengeneza jina, pambano lake la kwanza alipopokea fedha nyingi ni Sh1 milioni, ambayo ilimfanya achanganyikiwe kujituma zaidi.

KIDU 04 (1)

“Fedha hiyo nakumbuka nilipambana na bondia kutoka Afrika Kusini, Ramadhani Buru.”


DIAMOND, ALIKIBA

Kila mwanadamu ana starehe yake. Ukiondoa kipaji alichobarikiwa na Mwenyezi Mungu, kuna ambao ni wasanii wa kuigiza lakini wanapenda mpira, na kuna ambao ni wanariadha lakini wakimaliza majukumu yao kuna vitu wanapenda kufanya. Kwa upande wake Twaha anasema mbali na kupenda sana kazi yake ya ngumi, akipumzika anapenda kucheza bao au kusikiliza muziki.

“Mimi ni mdau sana wa muziki na napenda muziki mzuri. Mara nyingi napenda kusikiliza nyimbo za Diamond, Alikiba, Harmonize na Jay Melody. Ni wasanii ambao nimekuwa nikiwasikiliza sana,” anasema na kuongeza:

“Mimi sio mpenzi wa Hip Hop, napenda nyimbo laini. Ngumu sana hapana, japo kwenye muziki huo huwa namfuatilia sana Kontawa, ni msanii ambaye anajua sana. Huku nyumbani kwetu Morogoro kuna Stamina, ambaye pia nimeimba naye wimbo mmoja.”

Anasema wimbo alioimba na Stamina ukitoka, dunia itasimama. Anasema amekuwa akisumbuliwa na msanii huyo akimuhoji ni lini watautoa, akimtaja pia Belle 9 kuwa ni nembo nyingine ya Mkoa wa Morogoro.


BADO ANATAMANI MAFANIKIO

Twaha anasema kwa kiasi kikubwa amefikia yale aliyokuwa anayaomba, lakini bado anatamani kuendelea kufanikiwa zaidi.

“Mafanikio hayajawahi kutosha. Kwa asilimia kubwa, nimepata vitu vingi nilivyoviomba tangu nianze kupambana, Mungu kanijaalia mafanikio kwa kutimiza asilimia kubwa ya vitu vyote nilivyoviomba nimevipata,” anasema na kuongeza:

“Kipindi hicho nilikuwa sijui kama nitakuja kutoboa kwenye ngumi. Nilimuomba Mungu vitu vingi sana, namshukuru nimevipata. Na sisi wanadamu hatujawahi kutosheka kwenye mafanikio, tuna tamaa, haturidhiki. Kadri unavyopata mafanikio, unatamani kufanikiwa zaidi.”

Twaha Kiduku anasema bado anatamani vitu vingine zaidi licha ya kupata vile alivyokuwa anatamani kuwa navyo kipindi hicho.

KIDU 07

NIDHAMU NI MUHIMU

Twaha anaweka wazi kuwa mafanikio mengi aliyoyapata kwenye kazi yake yamechangiwa na nidhamu.

“Ukitaka kufanikiwa kwenye kila jambo, kuna vitu viwili muhimu sana vya kuzingatia — Mungu na nidhamu. Ukivifuata hivi vitu viwili utaweza kufanikiwa bila kujali unapitia magumu mangapi,” anasema na kuongeza:

“Kwa mabondia wote, mimi ni bondia mwenye nidhamu kubwa sana. Sijisifu, ukweli ndio huo. Kimekuwa nikimuheshimu kila mtu bila kujali. Nawashauri nyie waandishi, na pia watu wengine wote wawe na nidhamu kwenye majukumu yao ili waweze kufanikiwa.”


MAISHA HALISI NDIO RAHISI

Wakati kuna msemo usemao 'pata pesa tujue tabia yako', unaomaanisha wengi akipata pesa hubadilika tabia, kwa upande wa Twaha ni tofauti, kama anavyoeleza mwenyewe.

“Naamini katika kuishi maisha yangu na sio kutumia umaarufu wangu kujikweza. Napenda kuishi kawaida sana, maisha halisi ndiyo maisha rahisi. Namshukuru Mungu nimepata umaarufu, nimekuwa staa, lakini napenda sana kukaa vijiweni na nyumbani.

“Siwezi kuishi maisha yangu ya umaarufu na kumdharau mtu. Jina langu haliwezi kunibadilisha kuwa tofauti na wengine. Napenda kuishi na watu vizuri ili kesho na keshokutwa waweze kunisaidia nikikwama.”

Anasema kama upepo wake wa mafanikio ulianzia Morogoro, atahakikisha anaishi hapo. Hawezi kuyumbishwa na mafanikio na kuukataa mji aliokulia na kumtoa kimaisha.


AZAM FC, MAN U

Ukiondoa kupenda kazi yake ya kupigana, ambayo ndiyo ajira yake, Twaha ni shabiki mzuri wa soka, ambapo ameweka wazi kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Azam FC kwa timu za Ligi Kuu, lakini nje ya Tanzania, Ulaya, yeye ni shabiki wa Manchester United.

“Mimi ni shabiki mkubwa wa Azam FC, naipenda sana hii timu. Ikicheza napenda ipate matokeo. Bila wao nisingekuwa hapa nilipo; wameniheshimu, hivyo timu yao nitaitangaza kwa mazuri popote nitakapokuwapo.

“Kwenye kikosi cha timu hiyo, kipindi cha nyuma nilikuwa namkubali sana Prince Dube, ambaye sasa anacheza Yanga, lakini hilo haliondoi kuendelea kuisapoti Azam FC.”

Akizungumzia Man U, anasema ni timu ambayo amebaki nayo kwa sababu ya ushabiki tu, lakini haifuatilii sana kwa sasa kutokana na matokeo yake.

KIDU 06

MAREKANI MIAKA MITATU

“Kuna kipindi tulipata udhamini na Ibrahim Class, tukipata mkataba wa kwenda kuishi Marekani miaka mitatu. Nilivyouona huo mkataba, nakumbuka kipindi hicho nilikuwa tayari nimesafiri nchi mbili — Poland na Urusi — halafu ndipo nikapata huo mkataba,” anasema na kuongeza:

“Kutokana na mazingira, nikamwambia Ibrahim wewe nenda, mimi niache Bongo. Mwenzangu alienda, nakumbuka alikaa mwaka mmoja tu. Alivyorudi tu, akakuta mimi nishakuwa maarufu na nimepata vitu vingi. Akaniambia, ‘bora wewe ulivyogoma.’”

Kiduku anasema anaamini kuwa hana sababu ya kuhama sehemu ambayo imempa jina. Kwa kuhofia umaarufu alionao Morogoro, ndiyo kumemtambulisha. Ataishi huko, na ikitokea anatoka, basi anatoka na familia yake kwa siku kadhaa na kurudi.


NYUMBA, BODABODA, SALON

Kiduku anasema mbali na kupigana amewekeza nguvu zake kwenye uwekezaji.

“Ukiondoa mapambano, mimi nimefanya uwekezaji kwenye nyumba, bodaboda na saluni za kunyoa nywele. Kama hivi sasa ambavyo sipati promota ambaye ataniandalia pambano kwa kiasi cha fedha ninachotaka, najua wapi patanipa maisha,” anasema.

“Nina nyumba za kupangisha, bodaboda, lakini pia saluni za kunyoa... hizi ndizo zinanifanya maisha yangu yanaenda.”


UCHAWI UPO, HAUAMINI

Ushirikina upo, lakini kwa Tanzania kisheria hakuna anayeamini kwa sababu haina ushahidi. Hata hivyo, kwenye vitabu vya dini imeandikwa kuwa ipo, kama anavyofunguka Twaha Kiduku.

“Mganga Mungu tu, miti shamba imani. Kwenye pambano kila mmoja anaenda kutimiza imani yake. Mfano, kama mimi nilivyokutana na bondia mmoja, mashabiki wakawa wananitisha eti kuna 'kibabu kimefanya yake', lakini mwisho wa siku Mungu ndiye kila kitu, nikashinda pambano,” anasema na kuongeza:

“Hatumaanishi kwamba uchawi hakuna. Ndiyo maana sisi Waislam tunaamini kwamba uchawi upo, na Mtume wetu alilogwa. Hivyo ushirikina upo, dua zipo, tunamuomba Mwenyezi Mungu ili kutokuupa nafasi uchawi.”

KIDU 02

AZAM TV NA NGUMI

“Baba wa mchezo wa ngumi nchini ni Azam TV, wanaubeba sana mchezo huu. Tukubali tukatae, bila wao hakuna bondia atakayezungumzwa sana kwa ubora,” anasema na kuongeza:

“Wengine wapo, wanapambana kuunyanyua huu mchezo, lakini hawawezi kuifikia Azam TV. Ni chombo kikubwa ambacho kinautangaza mchezo ndani na nje. Kwa mfano, hata kwenye mafanikio yangu ninayojivunia, bila wao nisingeweza.”

Twaha anasema Azam TV imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuwaheshimisha mabondia, kupata maslahi na maendeleo kupitia mchezo huo, na kuondoa changamoto ya kumnufaisha promota pekee.

“Kuna muda mabondia walikuwa wanateseka na waliishia kuambulia hela ya kula tu, kwa sababu mapromota walikuwa wanawabana mabondia na kujinufaisha wao tu. Hadi bondia akija kustaafu anakosa cha kuonyesha kama mafanikio,” anasema na kuongeza:

“Kwa sasa Azam TV amerudi kuonyesha mapambano, lakini hatuwezi kuendelea tulipoishia. Tunaanza mdogo mdogo ili kuurudisha huu mchezo, ambao sasa ni ajira kwa vijana wengi.”