Neymar hatarini kukosa mechi zote Kombe la Dunia

Doha, Qatar. Brazil imeonyesha wasiwasi juu ya hali ya afya ya mshambuliaji wake, Neymar, kuwa huenda akakosa mechi zote zilizobaki za Kombe la Dunia.

Nyota huyo mwenye miaka 30, alitolewa uwanjani wakati wa mchezo wa kwanza wa Brazil dhidi ya Serbia kutokana na kuumia kifundo cha mguu.

Imefahamika kwamba ana tatizo katika kifundo cha mguu, ingawa madaktari wa timu ya taifa ya Brazil walisisitiza kuwa anakosa mechi za hatua ya makundi pekee.

Brazil iliendeleza mwanzo mzuri wa mashindano bila kuwa na Neymar, wakati Casemiro akifunga bao pekee la ushindi Jumatatu, wakati ilipoizamisha Uswisi kwa bao 1-0.

Lakini wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia kucheza bila Neymar, wakati taarifa zilizoandikwa na gazeti la The Mirror, likidai kuwa nyota huyo ana tatizo la msuli wa nyuma ya paja.

Tatizo hilo linamaanisha kwamba ni kubwa kuliko lilivyodhaniwa awali na linaweza uathiri kikosi cha Brazil kama kitaendelea kuamini juu ya uwezo wa nyota huyo kupata ushindi.

Lakini suala la ufiti wa wachezaji kwenye mashindano hayo si jambo jipya kwa Neymar, ambaye alikuwa akidaiwa kuwa na bahati mbaya linapokuja suala la fainali za Kombe la Dunia.

Katika fainali za 2014, alianza kwa kuonyesha kiwango bora nchini Brazil, lakini aliumia mgongo kwenye mechi ya robo fainali na kukosekana katika mchezo wa kipigo cha mabao 7-1 dhidi ya Ujerumani.

Miaka minne baadaye, aliingia katika Kombe la Dunia akiwa na tatizo la utimamu wa mwili na Brzil kutolewa na Ubelgiji katika hatua ya robo fainali.