We kamu umcheki Mandonga Mtu Kazi

TAMBO za bondia kutoka Bongo, Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ zimetikisa nchi kwa wiki nzima na leo katika Ukumbi wa KICC jijini Nairobi ni muda wa kutekeleza alichokisema atakapopanda ulingoni kupambana na bingwa wa zamani Afrika, Daniel Wanyonyi.
Pambano kati ya Mandonga na Wanyonyi litakuwa la utangulizi kabla ya pigano la wazi kati ya Rayton Okwiri na Mtanzania Shabani Ndaro ambaye hajapoteza mapigano yake matano yaliyopita. Hapo awali Okwiri alipangwa kupigana na Mkenya mwenzake Kassim Ouma lakini pambano hilo halikufayika nchini Uganda.
Tangu kuwasili kwake nchini siku ya Jumatano wiki hii, Mandonga amekuwa gumzo akiwapa tabasamu Wakenya mtandaoni kutokana na namna alivyokuwa anamtumia salamu mpinzani wake Wanyonyi ambaye naye amerusha cheche kali kwa Mandonga.
Akiwa katika eneo lake la biashara la Look Noma Noma soko la Gikomba katikati mwa jiji la Nairobi, alitembelewa na Mandonga kabla ya pambano lao. Hapo jana, wawili hao walipima uzito nje ya hifadhi ya taifa saa 10 asubuhi.


WANYONYI APATA BACK UP
“Haiwezekani kutegemea ndondi tu, huku barani Afrika maisha ni magumu kwa mabondia wengi, ndio maana nina upande wangu kutafuta riziki kupata mapato ya ziada,” alisema Wanyonyi ambaye amemtaja Mandonga kama kasuku lakini akamshukuru kwa huduma zake za uuzaji bila malipo katika pambano lao.
“Mandonga amefanya kazi nzuri sana kutangaza pambano letu, mbwembwe zake ni muhimu katika mchezo wa ndondi,” alisema Wanyonyi.
Bondia huyo Mkenya mwenye umri wa miaka 39, alisema Mandonga anaishi katika eneo la ndoto na kile anachotaja kama vitisho vyake vya kuuawa tupu.
“Atuambie ameua watu wangapi badala ya kutoa vitisho visivyo na msingi kwa bondia wa aina yangu, sina nia ya kumuua kwa vile ana familia lakini ajiandae kwa vita kamili,” alisema Wanyonyi.
Wanyonyi alishinda taji la Muungano wa Ndondi Afrika (ABU) ubingwa wa uzito wa Light-Heavy mwaka 2014 kwa pointi dhidi ya Matamba Debatch Postolo wa DR Congo lakini hakuwahi kuutetea mkanda huo tena.
Mashabiki wake wanamtaka eneo hilo la Gikomba wanamtaka Wanyonyi asimwache hata chedmbe Mandonga.
“Nashangaa Mandonga ana kelele lakini hili ni pambano lake la kwanza tu nje ya Tanzania. Anapaswa kwenda pole pole ajifunze taratibu, hatahivyo hayupo kwenye ligi yangu,” alitamba Wanyonyi.
Aidha anasema mpinzani wake huyo kutoka Tanzania, amekuwa akipigana na mabondia wachanga na leo ndani ya Ukumbi wa KICC anakutana na mtu aliyetahiriwa kabisa kutoka Uluyani.
Wanyonyi amewataka waliotwishwa jukumu la pambano hilo wawe waadilifu akisema ataenda raundi 10 kamili na Mandonga lakini kuna uwezekano mkubwa akamaliza pambano mapema.
“Siko tayari kwa njia za mkato, acha bondia bora ashinde vifiti lakini si kupitia njia yoyote ya mkato,” alisema.


MANDONGA AMEMBAMBA
Alipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Mandoga alilakiwa na mashabiki wake ambao walikuwa wanamsubiri kwa hamu.
Alikutana katika uwanja huo wa ndege na Katibu Mkuu wa Tume ya Ndondi za Kulipwa Kenya (KPBC), Franklin Imbenzi na promota wa Solid Rock, Mike Odongo.
“Wajue kuwa Mandonga ‘Mtu Kazi’ na sasa yuko Kenya na nimepokelewa vizuri, najiona bado nipo Tanzania. Wajue kwamba nitamfunza Wanyonyi somo, kwasababu ninahisi nguvu, siogopi chochote. Nimefanya kazi kwa bidii; wanaofanya kazi kwa bidii kama mimi hawajui kushindwa, hapana! Nimeleta ngumi niliyowaahidi Wakenya, ngumu iliyotengenezwa Ukraine, inaitwa ‘Sugunyo’. Ole wake mpinzani wangu,” alitamba Mandonga.
Mandonga alifanikiwa katika pambano lake la mwisho nchini Tanzania ambapo alimshinda mtani wake Said Mbelwa kwa TKO.
Bondia huyo wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 43, anafahamika kwa kauli zake za ucheshi kabla ya pambano na ameapa kumwangusha Wanyonyi huku akiahidi kuzindua mbinu mpya.
“Wanyonyi lazima tukupige tu! Unataka tunakupiga, hutaki tunakupiga! Hapa hapa Kenya,” aliwaambia wanahabari hapo jana.
“Mimi ni ripoti yake ya kwamba yeye ni mkongwe amecheza mapigano mengi lakini hana rekodi ni kibarua mgunda tu. Kupigwa atapigwa.”


WAKENYA WAMEMKUBALI
Mkenya mmoja kwa jina la Ms. Tasha Xclusive aliandika kwenye ukurasa wake wa kijamii,
“Mandonga yuko kwenye blogu zote za Kenya, anga za mitandao ya kijamii, kushoto na kulia na ni wazi timu yake ya kufanya kiki inafanya kazi. Halafu nashangaa kama Wanyonyi ana timu ya kusaidia kumuuza, au Wakenya wameridhika tu na kila kitu cha wastani kinachopatikana. Kisha watu watatuchukia kwa kuwaunga mkono watu wengine. Duh! Je, nakuunga mkono vipi wakati hakuna kitu kuhusu wewe kinachotokea POPOTE!! Dah Taifa letu hili,” aliandika Tasha.
Mkenya mwingine Kiarie Mbugua pia alisema, “Huyu jamaa Mandonga yuko mbali na kuwa bondia. Walakini, inavyoonekana, alikuja shuleni kwetu juu ya jinsi ya kujenga chapa zetu na kuwatangaza watu wetu wa michezo.”
Naye Mbunge wa Lang’ata ambaye pia ni mchekeshaji maarufu akifahamika zaidi kama Jalang’o aliandika, “Januari 14! Mandonga Mtu Kazi atakuwa Kenya! Ukijua ujue… Weeee... KICC JUMAMOSI KUTAWAKA! Mandonga amefika!!”
Shabiki mmoja shupavu wa Wanyonyi ambaye amekerwa na vitisho vya kifo cha Mandonga, Moses Muthee naye aliandika, “Tumeona mapambano lake, ni muoga, tutampiga sana, mtandao haudanganyi. Mandonga amesema ana vipigo vinavyojulikana kwa jina la Sugunyo kutoka Ukraine, sisi hapa ndio fire zaidi noma noma. Zetu zinaitwa Mfungukure idhaa ya ngori, atakiona Sato huyu msee wa mdomo.”


AMBULENSI IPO
Okwiri almaarufu ‘Boom Boom’, amewatahadharisha Mandonga na Ndaro kuwa mipango yao ya kulazwa hospitalini imekamilika maana hapotoki mtu.
“Tuko nyumbani, na watajua hawajui, wacha mikono itembee, chimba mtu mpaka apige magoti, Watanzania wamerusha mawe Polisi."
Okwiri atamenyana na Ndaro ikiwa ni mara yake ya kwanza kupigana nyumbani tangu Desemba 2019 alipomchuna bondia wa DRC, Augustine Matata kutetea taji lake la uzito wa kati la ABU.