Wambui: Simba Queens pananifaa

WING’A wa timu ya taifa ya Kenya wanawake maarufu Harambee Starlets, Elizabeth Wambui ambaye alijiunga na Simba Queens ya Tanzania, amesema timu nyingi zilitaka kumsajili lakini akaamua kwenda Bongo.

Wambui alijiunga na Simba Queens mwezi Novemba kwa maktaba wa miaka miwili akitokea Gaspo Women inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF-WPL).

Alizitaja timu zingine zilizokua zinamezea saini yake ni CBE ya Ethiopia na Buja Queens ya Burundi.

“Niliamua nije Tanzania kujiunga na familia ya Simba Queens ambao walinipokea vizuri hadi nikajihisi nipo nyumbani mbali na nyumbani. Ningependa kuwashukuru wachezaji wenzangu, benchi la ufundi na familia nzima ya Simba kwa ukarimu wao. Nina ahidi nitawatendea haki msimu huu,” alisema Wambui.

Kando na kuichezea Starlets, ameshaichezea japo kwa mkopo Agosti mwaka huu timu ya Buja wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika Uganda kwa ajili ya CECAFA kupata mwakilishi wa Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Olympic High kutoka jijini Nairobi, aliisaidia Buja kumaliza nafsi ya tatu katika mashindano hayo ya CECAFA.

“Kuchezea klabu za mataifa mengine nilipata kujifunza mengi na hilo lilinisaidia kukua kisoka. Kila timu ina kocha tofauti, ukufunzi tofauti na filosofia ni tofauti. Kila siku mazoezini najituma sana ilikuendelea kuwa bora,” alisema Wambui.