Wachungaji wakipata cha moto

TIMU ya wachungaji ya Mombasa West Pastors FC walishindwa kueneza neno kwa wazee  wa Chaani Youth Parents walipochezea kichapo cha mabao 3-2 kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa uwanja wa kisasa wa Bomu Changamwe, Kaunti ya Mombasa.

Mombasa West Pastors FC walipata mabao yake kupitia kwa Mchangaji Byram na Mchungaji Edward dakika za mwanzoni mwa mchezo.

Nao Chaani Youth Parents FC walipata mabao yao kupitia kwa mkufunzi wao Jones Kyalo aka coach Viera, Abubakar Kassim kwa njia ya penati na Peter Mutavi.

Wachungaji hao walijikuta katika kona mbaya kwenye mechi hiyo kutokana na kwamba wengi wao walidhihirisha hali ya uchovu mapema kabla mechi kushika kasi.

Kwenye mechi nyingine ya kirafiki katika uwanja huo huo, Mombasa West Pastors FC walirindimwa mabao 5-2 na timu ya Air Force FC kutoka eneo la Port Rietz.

Wanahewa waliweza kuwatuliza wachungaji kuanzia dakika za kwanza za mechi baada ya kipa nambari moja na mbili wa kikosi cha timu ya Mombasa West Pastors FC kuumia.

Mkufunzi wa kikosi cha wachungaji Pastor Edward amesema kikosi chake kinajizatiti kukabiliana na timu ambazo mara nyingi ziko katika mazoezi.

“Nia yetu ya kuunda timu ni kutaka kuwa karibu na jamii na kuionyeaha ya kuwa kazi yetu sio kuhubiri neno la Mungu pekee bali hata kuleta utangamano kupitia michezo,” alisema Pastor Edward.