Ukitaka unafungwa, usipotaka unafungwa

LIGI Kuu Kenya ni mwendo wa hakuna kulala mechi tisa zikiratibiwa kupigwa leo kwenye viwanja tofauti tofauti huku mbio za ubingwa zikiendelea kunonga.
FKFPL imekuwa bandika bandua ili kukimbizana na muda kuhakikisha ligi ya msimu huu inamalizika kwa wakati ikizingatiwa ilianza kuchelewa kutokana na klabu kususia kushiriki ligi ambayo haitambuliwi na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Tusker FC ambao walilazimishwa sare tasa na Nzoia Sugar, watawakaribisha FC Talanta katika Uwanja wa Ruaraka jijini Nairobi wakisaka kurudi kwenye hali yao ya ushindi baada ya mechi mbili za presha wakiambulia pointi moja tu.
Mabingwa hao watetezi watamkosa beki wao Tom Teka aliyeonyeshwa kadi ya pili ya njano katika mechi dhidi ya Nzoia Sugar na wanawakabili Talanta FC yake Ken Kenyatta iliyozinduka mwishoni mwa wiki kwa kutoka nyuma na kuichapa Mathare United mabao 3-2.
Mathare United ambayo ndiyo timu pekee haijaonja ladha ya ushindi, watakua ugenini Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi kuwakabili AFC Leopards ambao nao pia hawajakua na matokeo mazuri.
Ingwe walipoteza mchezo wao wa nne msimu huu Jumamosi wakifungwa mabao 2-1 na Wazito FC lakini kocha Patrick Aussems ameomba mashabiki kuwa wavumilivu kwani licha ya timu yake kupoteza imekua ikionyesha kandanda safi.
“Makosa mengi ya kibinafsi kwenye mechi mbili za mwisho lakini makos ani sehemu ya mchezo hivyo nitaendelea kuwapa sapoti na kuilinda timu yangu chipukizi ten ana tena,” alisema kocha huyo raia Ubelgiji.
Nzoia Sugar ambao msimu huu wamekuja kivyingine watakuwa kwenye uga wao wa nyumbani Sudi kaunti ya Bungoma kuwakaribisha Wazito FC iliyoshinda mechi zake mbili za mwisho.
Nao mabingwa wa kihistoria Gor Mahia ambao walipata ushindi mtamu kaunti ya Kakamega kwa kuwafunga wenyeji Kakamega Homeboyz wanawakaribisha Sofapaka ambao wamekua na msimu wa pandashuka.  
Bandari FC ambayo fomu yao imepanda wakishinda mechi mbili za mwisho dhidi ya Tusker FC na Vihiga Bullets, watakuwa wageni wa Ulinzi Stars ugani Ulinzi Sports Complex huku kocha Anthony ‘Modo’ Kimani akitaka vijana wake kuendeleza wimbi la ushindi.
“Ulinzi wanacheza kitimu na wachezaji wao ni wa viwango vya juu hivyo lazima tuwe na nidhamu katika kila idara na kutumia nafasi tunazozitengeneza,” alinukuliwa Kimani.