Uganda wamruka Namwamba kipetero, waitaja Tanzania

KWA mara nyingine tena, Waziri wa Michezo, Ababu Namwamba, alithibitisha mbele ya ujumbe wa FIFA uliofika nchini, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Mataifa Wanachama kutoka Afrika, Gelson Fernandes, kuwa Kenya ina mpango wa kushirikiana na nchi jirani za Afrika mashariki, Uganda na Tanzania, katika kuandaa makala ya mwaka 2027 ya michuano ya Kombe la Afrika (AFCON).

Hata hivyo, Waziri wa Michezo nchini Uganda, Peter Ogwang, amekana kuwepo kwa mpango wowote wa kuishirikisha Kenya akisisitiza mipango yao ya awali ni kuyaandaa mashindano hayo, sambamba na taifa la Tanzania.

Ogwang akikiri kuwepo kwa mpango kati ya Uganda na Tanzania na hajapata taarifa yoyote kuhusu ombi la Kenya kuungana nao.

“Sina taarifa yoyote kuhusu Kenya, ninachojua ni kwamba, Tanzania na Uganda, zinajiandaa kutuma ombi la pamoja,” alisema.

Taarifa ya Uganda, inathibitisha kauli ya awali ya Waziri Namwamba ambaye alikiri Jumatatu kuwa, licha ya kuweka mpango huo hadharani, Kenya bado haijawasiliana na Uganda, Tanzania ama mataifa mengine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tunajiandaa kutuma ombi la kuwa wenyeji wa AFCON 2027.  Tutashirikisha wale tutakaoona wana umuhimu katika mpango huu. Kwasasa, tunataka kuhakikisha kuwa, tuko tayari kwa ajili ya AFCON,” Ogwang alisema.