Stori ya Matasi kwisha

KUHUSU lile sakata la kipa bora wa msimu uliopita, Patrick Matasi, kutaka kuondoka Tusker FC, sasa limekwisha.

Matasi amekuwa akiitumia mbwembwe nyingi, ikiwemo kususia vikao vya mazoezi, ili kuishurutisha klabu hiyo imvunjie mkataba ajiunge na Police FC ambako ameahidiwa ajira kama ofisa polisi.

Lakini klabu hiyo imeamua haitamwachilia kipa huyo aondoke hata ikiwa atagoma kucheza.

Kocha Robert Matano ambaye wiki iliyopita aliiambia MWANASPOTI kuwa ishu hiyo ipo nje ya uwezo wake, sasa amebadilisha lugha baada ya kupata maelekezo mapya kutoka kwa uongozi.

Matano alikiri kuchochwa na vuta ni kuvute iliyopo baina ya Matasi na Tusker FC akiiomba klabu kumalizana na jamaa mapema ili aweze kuendelea na maandalizi ya kikosi chake bila usumbufu.

Kulingana na duru kutoka ndani ya klabu hiyo, uongozi wa Tusker FC umeamua hautaingia hasara na hata ikiwa Matasi atasusia kutumika uwanjani, basi wataendelea kumshikilia kwa mwaka wote mzima hadi pale mkataba wake utakapofika mwisho.

Mabingwa hai wanataka kulipwa ada ya Sh1 milioni ili kumwachia lakini Police FC waliwasilisha ofa ya Sh200,000 iliyokataliwa.

Utata wa Matasi umempelekea Matano kumsajili kipa wa zamani wa Bidco United, Brian Opondo, atakayeng’ang’ania namba na kipa chaguo la pili, Brian Bwire, na Michael Wanjala aliyepandishwa daraja kutoka kikosi chipukizi cha Tusker.