Simba Queens yakomba majembe Starlets

WACHEZAJI wawili wa Harambee Starlets straika Jentrix Shikangwa na beki Ruth Ingotsi Mukalukho wanatarajiwa kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, Simba Queens, kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Shikangwa, staa wa zamani wa Vihigi Queens, atajiunga na Simba akitokea timu ya Uturuki, Fatih Karagumruk SK baada ya mkataba wake wa muda mrefu na timu hiyo kusitishwa ghafla.

Naye Ingotsi, mchezaji wa zamani wa Eldoret Falcons, anajiunga na Simba Queens akitokea klabu ya Ligi Kuu ya Lacatamia yenye maskani yake Nicosia nchini Cyprus.

Meneja wa Simba Queens, Selemani Makanya, amethibitisha ujio wa wachezaji hao ambao anaamini wataisaidia mabingwa hao CECAFA kwenye michuano ya ndani nan je ya nchi.

“Tunajitayarisha michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake nchini Morocco baadaye mwaka huu na wachezaji hao watatusaidia kutokana na uzoefu wao,” alisema Makanya.

Shikangwa na Igotsi wanaungana na kiungo mshambuliaji Corazone Aquino, straika Topister Situma na kipa Carolyne Rufa ambao tayari walikuwa wamejiunga na klabu hiyo.