Shujaa ni kubaya, wahemea mchujo

KIKOSI cha taifa cha raga 7s, Shujaa kipo kwenye hatari zaidi ya kushushwa daraja mwishoni mwa msimu huu baada ya kuelendelea kuchemsha katika ligi ya dunia ya HSBC IRB 7s 2022/23.

Kwenye mkondo wa saba Hong Kong 7s wikendi iliyopita Shujaa waliendelea kuandikisha matokeo ya kufedhehesha baada ya kumaliza wa mwisho kwa kuzoa alama moja pekee.

Kwa ujumla baada ya kucheza mikondo minane, Shujaa wamekusanya jumla ya alama 30, pointi ambazo zimewaweka katika hali ngumu.

Ilivyo sasa, Shujaa wanachezea tundu la choo wakiwa karibu zaidi na upanga wa kushushwa daraja kuliko ilivyo nafasi yao ya kuponea, hususan ikizingatiwa zimesalia mikondo mitatu tu msimu huu kufika kikomo.


ITAKUWAJE SASA?

Tangu Shujaa walipoingia kwenye ligi hiyo 2004, hawajawahi kujikuta kwenye hatari hii hata siku moja kama ilivyo kwasasa.

Mikondo miwili ijayo ya Singapore 7s na Toulouse 7s, zitachangia pakubwa kuamua ikiwa Shujaa wanashushwa au wanabaki.

Kwa kuzingatia matokeo ambayo Shujaa wamekuwa wakisajili, fursa za kikosi hicho kuponea shoka la kuteremshwa daraja ni ndogo mno.

Ilivyo ni kwamba, kwenye mikondo hiyo miwili, ni lazima Shujaa wahakikishe wanatinga robo fainali ya Main Cup, ili kuepuka shoka hilo.

Kufika robo fainali kutawahakikisha angalau pointi 10 kutokana na kila mkondo, alama ambazo zitatosha kuwaokoa.

Na endapo Shujaa watafanikiwa kurudia matokeo waliyosajili 2016 waliposhinda Singapore 7s kwenye mkondo huo, basi watakuwa salama zaidi kwani watazoa alama 22. Lakini hilo kwa namna ambavyo kikosi kimekuwa kikifanya, ni sawa na ndoto za alinacha.


MCHUJO UPO HIVI

Timu yeyote itakayomaliza katika nafasi ya 15 baada ya mikondo kumi kuchezwa, itachujwa moja kwa moja kutoka kwenye ligi ya IRB 7s kuelekea msimu wa 2023/24.

Shujaa kwasasa wapo katika nafasi ya 13, wakifuatiwa na Canada 14 na Japan 15. Uhispani ambao pia wapo hatarini wanakamata nafasi ya 11.

Baada ya timu ya mwisho kuondolewa baada ya mkondo wa Toulouse, zile zitakazomaliza katika nafasi ya 11 hadi 14 zitaingia kwenye raundi ya mchujo kwenye mkondo wa 11, London 7s. Raundi hiyo ya mchujo itafahamika kama Challenger Series.

Timu hizo 11 hadi 14 zitachuana kwa kuzungukana. Timu mbili zitakazozoa alama nyingi zitachuana tena na mshindi ataepuka kuteremshwa daraja.

Zile timu mbili zitasukumwa kushiriki ligi za kanda zao almaarufu Regional Sevens Championships.


MKAKATI KUIKOA SHUJAA

Mwenyekiti mpya wa Shirikisho la Raga nchini (KRU), Alexander ‘Sasha’ Mutai, anasema kwamba tayari ameanza mpango kazi wa kuhakikisha Shujaa hawashuki.

“Kiwango cha kikosi kimekuwa kikiporomoka tangu mwaka jana na sasa hivi tupo kwenye hatari ya kuchujwa. Tatizo letu kubwa limekuwa ni maandalizi mabovu msimu wote huu,” Mutai anasema.

Ili kuokoa hali, Mutai anasema alikutaka na kocha Damain McGrath kuja na mkakati wa kuinusuru timu.

“Nilikutana na kocha wiki iliyopita na tukaafikiana kuiweka timu kwenye kambi ya mazoezi. Kikosi kilikuwa kikitumia uwanja wa RFUEA ambao hauna vifaa vya kutosha vya mazoezi. Kwasasa kuna unafuu baada ya kukihamisha hadi Moi Sports Center Kasarani ambako kuna vifaa vya kutosha. Kingine ni kuwa tumekiweka kikosi kwenye kambi ya pamoja,” anasema Mutai.

Ishu nyingine ni mkakati wa kumleta kocha wa misuli. Shujaa wamekuwa wakitaabika sana kwa kumkosa kocha mwenye utaalamu huu.

Mchakato wa kumleta mchezaji wa zamani wa kikosi cha Uingereza James Rodwell kusaidia kutatua upungufu huo unaendelea.

Aidha kocha mwenye tajriba ya mbinu za upigaji frikiki anasakwa kukipiga kikosi jeki. Shujaa tayari wamesafiri hadi Singapore kwa ajili ya mkondo hujao utakaochezwa wikendi hii.