Dabi ya Mashemeji...   K'Ogalo yaizamisha tena Ingwe

BAO pekee la dakika 30 lililowekwa kimiani na Austine Odhiambo limeiwezesha Gor Mahia kuizamisha tena AFC Leopards katika pambano la Dabi ya Mashemeji lililopigwa jioni ya leo Jumapili, jijini Nairobi.

Dabi hiyo ya 95 kwa timu hizo tangu Mei 5, 1968 lilipigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, huku wenyeji K'Ogalo ikicheza pungufu baada ya mchezaji mmoja kulimwa kadi nyekundu dakika 10 kabla ya mapumziko.

Pambano hilo la raundi ya 27 la Ligi Kuu ya Kenya, limeifanya Gor kuzidi kujikita kileleni ikifikisha pointi 57, huku Ingwe ikisalia nafasi ya nane na pointi 38.

Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Oktoba mwaka jana, Leopards ikiwa wenyeji ilinyukwa mabao 2-0.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizopigwa pia jioni ya leo Ulinzi Stars ikiwa nyumbani iligongwa bao 1-0 na Tusker, huku Muranga na Muhoroni Youth zikishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu.

Ushindi wa Tusker umeifanya ifikishe pointi 46 na kushika nafasi ya tatu.